.

.

.

.

Monday, June 27, 2011

BABU WA LOLIONDO AZAWADIWA GARI

MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapile wa kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro, ambaye anatoa dawa ya kutibu magonjwa sugu maarufu kama ‘Kikombe cha Babu’, amezawadiwa gari na mgonjwa aliyepona baada ya kunywa dawa yake.

Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM), ameliambia Bunge mjini Dodoma alipokuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa mwaka ujao wa fedha.

Telele amesema, Mchungaji Mwaisapile amekabidhiwa gari hilo aina ya Toyota Hilux Pick-up namba BL 9238 lililotolewa na mgonjwa huyo ambaye hakumtaja jina lakini ni raia wa Malawi anayeishi jijini Blantyre.

Amesema, Babu analitumia gari hilo kwenda kufuata dawa ambayo sasa inapatikana mbali kidogo kwa kuwa, katika maeneo ya karibu imemalizika kutokana na wingi wa wagonjwa.

Mbunge huyo alisema ingawa suala la dawa hiyo kuponya au kutoponya ni la mgonjwa mwenyewe, lakini dawa ya Babu imeipatia sifa kubwa wilaya ya Ngorongoro na kuifanya “kuwa juu kama mkungu wa ndizi.

“Mimi nawaomba wale waliokunywa dawa ya Babu waendelee kupima afya zao mara kwa mara, kama ambavyo Serikali imekuwa inasisitiza na napenda kuwapongeza sana wabunge wenzangu waliomo humu ambao walifika Samunge kupata ‘kikombe cha Babu’,” alisema Terere.

Hata hivyo Mbunge huyo alisema umaarufu wa Mchungaji Mwaisapile ambao umejulikana dunia nzima sasa, umelifanya Taifa la Kenya kumtumia ili kujiingizia mapato kwa kusema uongo, kwamba Mchungaji huyo anapatikana kijiji cha Samunge Kusini mwa Kenya.

Alisema upotoshaji huo ambao umekuwa ukifanywa kwa makusudi, umewafanya wagonjwa wengi wanaotoka mataifa mbalimbali duniani, kusafiri hadi katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Jomo Kenyatta, Nairobi au cha Williamson badala ya kushukia kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).

“Wanadanganya kwamba wagonjwa wakishuka KIA hadi Samunge ni kilometa 800 lakini wakishuka Nairobi au Williamson wakapita Narok hadi Samunge ni kilometa 45 tu wakati ni uongo, kwani kuna zaidi ya kilometa 300 kufika Samunge,” alisema Terere.

Aliitaka Serikali pamoja na kukanusha upotoshaji huo, lakini pia izuie hatua ya magari yanayobeba wagonjwa wanaopitia Kenya kuingia nchini na kwenda moja kwa moja Samunge bila kuzuia, wakati yangekuwa ni magari ya Tanzania yanaingia Kenya, yangezuiwa mpakani na wagonjwa wangehamishiwa kwenye magari ya Kenya.

No comments:

Post a Comment