.

.

.

.

Thursday, June 09, 2011

BAJETI YA SERIKALI TANZANIA 2011/2012


SERIKALI imetangaza Bajeti kwa 2011/2012 ya Sh 13.5 trilioni ambayo imetaja mambo manne ya msingi ya kupunguza makali ya maisha, lakini kama kawaida ikipandisha bei ya vinywaji baridi, bia na pombe kali huku ikitenga asilimia 14 ya bajeti yote kulipa Deni la Taifa. Vilevile, imeongeza adhabu ya kosa la barabarani kutoka Sh 20,000 hadi Sh 50,000.

Katika mchanganuo huo wa kibajeti, Serikali imetaja mambo hayo manne kuwa ni pamoja na maboresho ya sheria za kodi, kuongeza nguvu za uwekezaji katika sekta ya umeme na kupunguza bei ya mafuta ya petroli, kupunguza matumizi ikiwamo ukubwa wa misafara ya safari za viongozi na kuongeza fedha kwa sekta tano za kipaumbele.

Akisoma bajeti hiyo mjini Dodoma ambayo asilimia 65 imekwenda katika maeneo 15 ya kisekta ikiwemo ulinzi, Waziri wa Fedha na Uchumi, alifafanua kwamba mipango yote imezingatia kwa kina mawazo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Maeneo ya vipaumbele
Akitangaza maeneo hayo, Mkulo alisema katika bajeti hiyo miundombinu ya barabara, reli, bandari na mkongo wa mawasiliano wa taifa imetengewa Sh 2,781.4 bilioni ikilinganishwa na Sh1,505.1 bilioni za mwaka 2010/11 sawa na ongezeko la asilimia 85, lakini kwa mchanganuo wa kisekta ujenzi pekee imepewa asilimia 11.06.

Katika mchanganuo huo wa kibajeti, nishati na madini imetengewa Sh539.3 bilioni ikilinganishwa na Sh 327.2 bilioni za mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 65 na

maji imetengewa Sh 621.6 bilioni ikilinganishwa na Sh397.6 bilioni mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 56, kilimo na umwagiliaji kimetengewa Sh926.2 bilioni ikilinganishwa na Sh903.8 bilioni za mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.

Kwa kuchanganya na maeneo hayo ya vipaumbele, maeneo mengine ya kisekta yanayotarajiwa kutumia kiasi hicho cha asilimia 65 ya bajeti ni deni la taifa Sh1,901,850,995,000 sawa na asilimia 14.06, Hazina, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ulinzi na Ofisi ya Rais.Maeneo mengine ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Wizara ya Fedha.

Kupunguza manunuzi, posho, safari za nje
Mkulo alikiri kila mwaka Serikali inatumia sehemu kubwa ya bajeti yake katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali.

„Hivyo, katika mwaka wa fedha 2011/12, Serikali imedhamiria kuweka mfumo wa ununuzi wa umma unaowezesha Serikali na Taasisi zake kupata bidhaa na huduma zenye ubora unaotakiwa kwa bei nzuri,” alisema

Aliweka bayana kwamba, Serikali itaendelea na juhudi zake za kudhibiti matumizi yake kwa kusitisha ununuzi wa magari ya aina zote isipokuwa kwa sababu maalum na kwa kibali cha ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Mkulo alisisitiza, ”Kusitisha ununuzi wa samani za ofisi hususan zile zinazoagizwa nje ya nchi; kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyokuwa na tija; kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya Serikali; kupunguza safari za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na ukubwa wa misafara.”

Alisema katika mkakati huo, alisema Serikali itaendelea kupunguza uendeshaji wa semina na warsha isipokuwa pale inapobidi na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na kupunguza gharama za maonesho na sherehe mbalimbali.

Adhabu barabarani Sh 50,000, sigara, bia juu
Katika marekebisho hayo madogo ya sheria, Mkulo alitangaza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya zana za kilimo zifuatazo ambazo ni pamoja na mashine za kukausha na kukoboa mpunga, mashine za kupandia mbegu na matrekta ya kukokota kwa mkono .

Bajeti hiyo pia imetangaza msamaha wa VAT vifaa vya kwenye chakula cha kuku (NASCOR Pellet Feed) na kwamba hatua hiyo ina lengo la kuhamasisha uwekezaji katika ufugaji wa kuku nchini

Alitangaza msamaha pia wa VAT kwenye nyuzi za uvuvi (Nylon Fishing Twine) zinazotumika kutengeneza nyavu za kuvulia samaki hatua ambyo inalenga katika kupunguza gharama za uzalishaji na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini, kusamehe VAT kwenye vipuri vya mashine za kunyunyiza na kutifua udongo (sprayers and harrows) na mashine za kupanda nafaka (grain conveyors).

“Kuanzisha utaratibu wa marejesho ya kodi kwenye mauzo ya rejareja kwa bidhaa za ndani zinazouzwa kwa abiria ambao sio raia wa Tanzania wanaosafiri nje ya nchi. Utaratibu huu utaanza kutekelezwa kwa kuanzia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa mauzo ya thamani ya Sh400,000 na zaidi,” alitangaza Mkulo.

Alisema utekelezaji wa utaratibu huo mpya utaanza rasmi Januari 1, 2012.
“Napendekeza pia kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kwa nia ya kuongeza mapato na kuhamasisha mashirika na taasisi mbalimbali ziweze kuchangia katika juhudi za Serikali za kuboresha huduma katika sekta ya elimu,” aliongeza.

Mkulo alitangaza kuondoa msamaha wa VAT kwenye kuuza na kupangisha majengo ya kuishi ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuondoa unafuu wa VAT katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Non Governmental Organizations) na kuweka bayana, “ Hatua ii haitazihusu Taasisi za Kidini (Religious Organizations.

Mkulo pia alipendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 ili kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa Serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya Serikali

Mkulo alisema Serikali itarekebisha kwa asilimia 10 viwango vya ushuru wa bidhaa mbalimbali isipokuwa zile za mafuta ya petroli kama ifuatavyo: -
Vinywaji baridi kutoka Sh63 kwa lita hadi Sh69 kwa lita,
bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka Sh226 kwa lita hadi Sh249 kwa lita, na kuongeza bia nyingine zote, kutoka Sh382 kwa lita hadi Sh420 kwa lita.

Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka Sh1,223 kwa lita hadi Sh 1,345 kwa lita, mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 utatozwa Sh420 kwa lita.

Vinywaji vikali, kutoka Sh1,812 kwa lita hadi Sh1,993 kwa lita, kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo, sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh6,209 hadi Sh6,830 kwa sigara 1000.

Mkulo alisema sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh14,649 hadi Sh16,114.
Pia alisema kwamba sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) zimepanda kutoka Sh26,604 hadi Sh29,264 kwa sigara 1000.Waziri Mkulo pia alipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Leseni ya Biashara, ili kutoza ada ya leseni ya biashara kwa viwango na maeneo mbalimbali.

Waziri Mkulo alitaja maeneo hayo kwamba ni pamoja na ada katika Mamlaka za Miji (Majiji, Manispaa na Miji) ambazo zitapaswa kutoza Sh50,000 kwa mwaka kwa kila aina ya biashara inayostahili kupewa leseni ya biashara (isipokuwa ya vileo) inayoendeshwa katika maeneo ya mamlaka hizo.

“Halmashauri za Wilaya zitoze na kukusanya ada ya leseni ya biashara ya Sh30,000 kwa mwaka kwa biashara zinazoendeshwa katika maeneo ya miji midogo na vituo vya biashara,”alifafanua Mkulo.

Katika mpango huo, alisema halmashauri za vijiji zitoze na kukusanya Sh10,000 kwa mwaka kwa kila biashara inayoendeshwa katika maeneo yake.

“Lengo la hatua hii ni kuimarisha usimamizi wa kanuni za biashara hapa nchini na kuwianisha ukuaji wa biashara na mapato yanayokusanywa. Pia itaongeza mapato kwa Serikali za Mitaa na kuongeza uwezo katika kuhimili mahitaji yao,” aliongeza Mkulo.

Katika marekebisho hayo, Waziri Mkulo alitangaza kugusa pia Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sheria ya Ushuru wa Stempu, Sheria ya ushuru wa Mafuta ya Petroli na Sheria ya Leseni za Biashara.

Sheria nyingine zilizoguswa ni pamoja na ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Usalama Barabarani ambayo ndiyo imeongeza adhabu ya faini kutoka Sh 20, 000 kwa kosa moja hadi Sh50,000.

Elimu ya Juu
Eneo jingine ni marekebisho kwenye sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ambayo Mkulo alisema lengo ni kuwezesha mgawanyo wa mapato yatokanayo na tozo la kuendeleza ufundi stadi (Skills Development Levy) ya asilimia sita, ili asilimia nne zipelekwe kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na asilimia 2 zipelekwe Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Vocational Education and Training Authority - “VETA”).
“ Lengo la hatua hii ni kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” alifafanua Mkulo.

Mfumo wa Bajeti
Alisema kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, inaonesha jumla ya Sh13,525.9 bilioni zinahitajika kutumika katika kipindi cha 2011/12.

Akitoa mchanganuo huo, alisema jumla ya mapato yanayotarajiwa ni Sh 13,525.9 bilioni ambazo kati ya hizo , Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh 6,775.9 bilioni, sawa na asilimia 17.2 ya Pato la Taifa.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment