.

.

.

.

Thursday, June 30, 2011

CHADEMA YASEMA SHIBUDA NI MSALITI


KITENDO cha Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda kupingana na sera ya chama chake kuhusu suala la posho za vikao (sitting allowance), kimeichefua Chadema ambayo imemuita msaliti ikisema, "adhabu yake ni kufukuzwa."Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliliambia Mwananchi mjini Dodoma jana kuwa, alikerwa na kauli iliyotolewa na Shibuda ya kwenda kinyume na msimamo kambi hiyo kupinga posho za vikao kwa wabunge na wafanyakazi wengine wa umma.

Mbowe alisema kwamba kwa kauli yake ya juzi ya kuunga mkono posho ilidhihirisha kwamba mbunge huyo ni msaliti wa kambi hiyo, hivyo sheria zitafuata mkondo wake.

"Kutokana na tukio la jana (juzi) bungeni, Shibuda kutusaliti katika suala la posho za vikao, taratibu za kisheria zitafuata mkondo wake kwani utovu wa nidhamu haukubaliki katika kambi yetu, hata katika chama chetu,"alisema Mbowe na kuongeza:

"Suala la posho si la mtu binafsi, lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi wa 2010 ya chama chetu na kama kuna kiongozi hafahamu hili basi hakustahili kugombea ubunge kwa sababu naamini Ilani ya Uchaguzi, Shibuda anayo."

"Posho zilijadiliwa na kupitishwa katika vikao maalumu vya chama, kwa hiyo kama Katiba yetu ya chama inavyotuongoza, Shibuda alitakiwa kulipinga katika vikao hivyo sio kutoka nje ya kikao na kuanza kupingana na maamuzi yake,"alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.


Akinukuu kifungu katika Katiba ya chama chake kinachoeleza maadili ya viongozi, Mbowe alisema, "Kiongozi anatakiwa kutii na kutimiza maagizo anayopewa na viongozi wa ngazi ya juu au vikao halali na kama hakubaliani na maagizo hayo aeleze hivyo kwa kupitia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye kanuni."

No comments:

Post a Comment