.

.

.

.

Thursday, August 04, 2011

KASHFA YA UFISADI UDA

KASHFA ya uuzaji kinyemela mali na hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limechukua sura mpya, baada ya jana Serikali kuombwa kuwakamata mara moja, Meya ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Idd Simba na wote waliohusika katika uuzaji wa mali za shirika hilo.

Wengine waliotajwa wakamatwe ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bakari Kingobi, Meneja Mkuu, Victor Milanzi na wakurugenzi wengine.

Ombi hilo lilitolewa bungeni jana na Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM) , wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi iliyosomwa jana na Waziri Omar Nundu aliyeomba kuidhinishiwa Sh 237,563,802,000 katika mwaka huu wa fedha.

Mbunge huyo, alisema ni aibu kuendelea kusikiliza jinsi UDA ilivyouza hisa na mali zake kihuni tena kwa fedha kupitia katika akaunti za watu binafsi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti (wa kikao cha Bunge), mwombe Waziri Mkuu atoe amri wakamatwe na kutiwa ndani bila kujali nani ni nani,” alisema na kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuivamia UDA na kuikagua.

Aliitaka pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) `kung’ata’ katika suala hilo. Shah alisema ni aibu kwa taasisi kupitisha fedha kwenye akaunti ya mtu binafsi kwa maelezo kuwa, UDA inadaiwa na benki na hivyo kuhofia zingeishia kwenye makato ya benki.

Alisema badala ya kukaa kimya wakati mali za umma zinauzwa, ni vema UDA irejeshwe mara moja mikononi mwa Serikali na iwe mmiliki kwa asilimia 100.

“Ni aibu wameuza hadi eneo la maegesho ya magari ya Kurasini kiasi cha Sh bilioni 1.4, si wangepewa hawa wenzetu akina Abood (Aziz) na Shabiby (Ahmed) wakapaendeleza badala ya kuuza kwa bei ya kutupa! Wameuza kiwanja pale stesheni, nyumba na mali nyingine,” alisema Shah aliyeunga mkono uamuzi wa kuzuiwa kutolewa hati mpya za umiliki wa viwanja vilivyouzwa na watendaji hao wa UDA.

Kabla Shah hajawasilisha ombi hilo, akisoma taarifa ya Kamati ya Miundombinu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema Kamati yake imeunda kamati ndogo ili kufuatilia sakata la UDA na taarifa ya ufuatiliaji itatolewa katika mkutano wa tano wa Bunge.

Kamati hiyo pia ilishauri Serikali kufanya tena mapitio ya mkataba wa mauzo ya hisa zilizogawiwa ulioingiwa kati ya UDA na kampuni ya Simon Group.

Dk, Charles Tizeba, Mbunge wa Buchosa (CCM), alihoji ujanja uliofanywa katika kuipiga bei UDA na kuhoji alikokuwa msimamizi wa mali za Serikali wakati `madudu’ hayo yakifanyika.

“Kutokana na taarifa zilizowasilishwa kwenye vikao, kamati imebaini utendaji wa UDA umeendelea kuzorota na kuna dalili za ubadhilifu wa mali na mapato ya shirika hili, kwa mfano mchakato wa kuendelea kuuza hisa za Serikali umeonekana kuwa na shaka,” alisema Serukamba aliyepongezwa na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Msemaji wa Upinzani katika wizara hiyo, Mhonga Ruhwanywa, alisema mchakato wa kuuzwa hisa za Serikali za UDA, umekiuka taratibu za UDA na sheria kwa kuwa mbia muhimu, yaani Serikali hakushirikishwa.

No comments:

Post a Comment