.

.

.

.

Wednesday, August 03, 2011

MAFUTA YAPUNGUZWA BEI !!!!!

BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa imepunguzwa kwa kiasi na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Kwa mujibu wa tangazo la Ewura jana kwa waandishi wa habari mjini hapa, bei hizo mpya zimeisha anza kutumika nchini kote.

Bei hizo zinaonesha kwamba, bei ya petroli imepungua kwa Sh 202.37, sawa na asilimia 9.17, dizeli kwa Sh 173.49(8.31%) wakati mafuta ya taa, yameshuka kwa Sh 181.37 (8.70%). Mabadiliko hayo yalitangazwa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, aliyesema bei mpya zimezingatia mapendekezo ya marekebisho ya vipengele vya kanuni ya kukokotoa bei za mafuta na hivyo kufanya punguzo kubwa la tozo katika biadhaa za mafuta.

Kwa mujibu wa Masebu, tozo katika petroli imepunguzwa kutoka Sh 54.03 kwa lita hadi Sh 27.27 (asilimia 49.53); dizeli kutoka Sh 55 hadi Sh 28.15 kwa lita (asilimia 48.80); mafuta ya taa kutoka Sh 55.66 hadi Sh 24.50 (asilimia 55.98). Kwa wastani, tozo za taasisi zimepungua kwa asilimia 51.44.

Kutokana na hatua hiyo, Ewura iliagiza, kwamba hakuna muuzaji wa rejareja atakayeruhusiwa kuuza petroli kwa zaidi ya Sh 2,004. Awali, bei ya juu kabisa ilikuwa Sh 2,206. Hali kadhalika, bei ya juu ya dizeli sasa ni Sh 1,910.84 ikilinganishwa na Sh 2,084 iliyokuwa ya kikomo mwezi jana.

Aidha, bei ya juu ya mafuta ya taa sasa itakuwa Sh 1,904.53 ikilinganishwa na ya awali Sh 2,085.90. Kutokana na bei mpya za bidhaa za mafuta, Masebu alisisitiza kwamba mfanyabiashara atakayeongeza hata senti moja, kosa hilo litamgharimu Sh milioni 3.

Hata hivyo, alisema katika kukabiliana na ushindani wa biashara, wafanyabiashara wanaweza kupunguza bei za bidhaa zao kiasi wanachopenda, ili kuvutia wateja, lakini si kuongeza bei.

“Nasisitiza, kuwa ni kinyume cha sheria kwa wauzaji bidhaa za mafuta kuuza kwa bei ya juu, tofauti na iliyopangwa na Mamlaka. Hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watakaokwenda kinyume na haya,” alisema Masebu aliyeahidi kufuatilia kwa karibu ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara.

Mkurugenzi huyo pia alionya wafanyabiashara watakaokwepa kuanza kutumia bei hiyo kuanzia leo, akisisitiza lazima zitumike, bila kujali mfanyabiashara ameingiza lini sokoni bidhaa yake na kwa bei ya wakati gani.

Aliongeza kwamba, Ewura ingependa kushusha zaidi bei ili kumpa nafuu mtumiaji wa kawaida, lakini kwa bahati mbaya kwa kiasi kikubwa bei ya bidhaa hizo inategemea na kupanda kwa bei katika soko la dunia na pia kuyumba kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

“Pamoja na kupungua kwa bei ya mafuta nchini, bado tuna changamoto, ikiwa ni pamoja na hii ya soko la dunia. Hata hivyo, Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” alisema.

Aliongeza kwamba viwango vya gharama za kibiashara vimezingatiwa ili kuhakikisha wafanyabiashara wanarejesha gharama zao za uwekezaji, uendeshaji na faida stahiki, huku mlaji naye akipata unafuu wa bei za bidhaa kwa ubora na ujazo unaostahili.

Ewura pia ilivitaka vituo vyote kuweka bei za mafuta katika mabango ya wazi yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na kwamba kinyume chake, adhabu kali zitamwangukia mmiliki wa kituo.

Aidha, wanunuzi wameshauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi za malipo zikionesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, ili stakabadhi hizo ziweze kutumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutatokea malalamiko ama ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au atakuwa ameuziwa mafuta yasiyo na ubora stahiki.

No comments:

Post a Comment