.

.

.

.

Monday, August 08, 2011

WANAOJIFUNGUA WATOTO ZAIDI YA WAWILI KUSAIDIWA

WABUNGE wametaka fedha zinazotengwa kusaidia wazazi waliojifungua zaidi ya watoto wawili kwa mpigo ziongezwe ili kutoa unafuu wa maisha kwa wazazi hao.

Wabunge hao walitoa hoja hiyo baada ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, alipokuwa akijibu swali, kueleza kuwa Serikali kwa sasa inalipa Sh 150,000 tena mara moja tu, kusaidia wazazi wa aina hiyo, kumudu matunzo ya watoto hao.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ritta Kabati (CCM) alisema fedha hizo ni kidogo na kuitaka Serikali kuziongeza huku akitaka kujua kama wazazi waliojifungulia majumbani hasa katika maeneo ya vijijini wanapata haki hiyo.

Naye Mbunge wa Mbozi, Godfrey Zambi (CCM), aliitaka Serikali mbali na kuongeza fedha hizo, pia ziwekwe kisheria ili iwajibike kuzilipa kwa kuwa kwa sasa zinaonekana kutolewa kama hisani.

Akijibu hoja hizo, Dk. Nkya alikiri kuwa fedha hizo ni kidogo, lakini akafafanua kuwa kwa sasa ni angalau ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Katika miaka hiyo; 1985 mpaka 1988, walikuwa wakilipwa Sh 10,120; 1989 mpaka 2001, walilipwa Sh 32,000 na malipo ya sasa ya Sh 150,000 yalianza kutolewa mwaka 2003.

Dk. Nkya alifafanua kuwa uchache wa malipo hayo, unatokana na fungu dogo la fedha lililowekwa katika bajeti ambazo mwaka uliopita wa fedha zilitengwa Sh milioni tano na mwaka huu zimetengwa Sh milioni saba tu.

Hata hivyo, alizitaka Halmashauri mbalimbali kutenga fedha katika bajeti zao za kusaidia wazazi hao ambao hujifungua watoto wengi kuliko matarajio na kujikuta na mzigo mkubwa wa malezi.

Kuhusu haki za wanaojifungulia nyumbani hasa maeneo ya vijijini, Dk. Nkya alizitaka kamati za afya katika vijiji, kutoa taarifa za wazazi wa aina hiyo, ili wapewe fedha hizo.

Pia aliwataka wazazi watakaopata msaada huo, kuzitumia kuanzisha miradi midogo ya maendeleo kwa ajili ya kujiongezea kipato na kupunguza ugumu wa maisha katika malezi.

No comments:

Post a Comment