.

.

.

.

Wednesday, December 21, 2011

JIJI LA DAR-ES-SALAAM LAKUMBWA NA MAAFA YA MAFURIKOPicha za angani zikionyesha maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yaliyokumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini humo.JIJI la Dar es Salaam na vitongaji vyake, limekumbwa na maafa ya vifo vya watu watano akiwamo mmoja aliyepigwa na radi, uharibifu wa miundombinu huku mamia ya watu wakikosa makazi, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.Mvua hizo zilisababisha tatizo kubwa la usafiri kutokana na barabara kujaa maji, kuezua nyumba na kuua watu watano na kuacha maelfu ya wakazi wa jiji hilo bila makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa mapaa.

Mvua hiyo ilianza kunyesha mnamo  saa 9:00 alfajiri ikiambatana na radi na ngurumo nzito na kusababisha kukatika mara kwa mara kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo ambalo ni kitovu kikuu cha biashara na uchumi kwa nchi.

Waandishi wa habari waliotawanyika sehemu mbalimbali za jiji hilo, walishuhudia maiti za watu wawili waliozolewa na maji maeneo ya Sinza na Msewe.

Wakati maiti moja ikitambuliwa kwa jina la Ibrahimu Lusama (60), maiti nyingine ambayo ilipatikana katika Bonde la Mto Ng'ombe bado haijatambuliwa.

Hata hivyo, moja ya maiti hao alisemekana anatoka eneo la Msewe na aliokotwa eneo la Sinza Iteba, takriban umbali wa kilometa tano. Madaraja ya Msewe na Sinza Iteba yalivunjika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wanaotumia madaraja hayo.

Madaraja mengine yaliyovunjika ni pamoja na daraja la Msewe na la mto wa Ng’ombe, huku magari yaliyokuwa yakienda Mwananyamala, Mikocheni yakitokea Ubungo yakilazimika kusitisha safari zake baada ya kujaa maji.

Baadhi ya maeneo ya jiji hasa Kigogo, Tandale, Mabibo na Tabata yalikumbwa na kadhia ya maji kujaa kwenye makazi yao na kusababisha usumbufu ambao ulionekana kutishia usalama wa mali na maisha.

Wazee walikuwa wakihangaika huku na kule kutafuta sehemu za kujisitiri, lakini vijana na watoto walionekana wakicheza kwenye mvua bila kujali mustakabali wao.

Wafanyabiashara wa vyakula vya jumla na rejareja katika baadhi ya maeneo waliamka na kukuta sehemu kubwa ya bidhaa zao zimeharibika huku meza na vyombo vya mama lishe, vikionekana kuelea barabarani baada ya kusombwa na maji.

Sinza
Mawasiliano ya Sinza na Tandale yalikatika baada ya daraja kusombwa na maji huku maiti ya mtu aliyeonekana kuwa mzee wa makamo ukikutwa umekwama kwenye kingo za daraja, kabla ya kuokolewa na wasamaria wema.

Mmoja wa wamiliki wa zahanati moja iliyoko Kigogo Darajani ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alisema  amepata hasara baada ya maji kuingia ndani na kuharibu vifaa mbalimbali vya hospitali zikiwamo dawa.

"Angalia, nimepata hasara sana. Mpaka sasa wasaidizi wangu wanafanya kazi ya kuzoa maji na kusafisha vitanda na baadhi ya vifaa, vingine havifai," alisema mmiliki huyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina.

Katibu wa CCM tawi la Kigogo Wakereketwa, Charles Gumbo alisema kulikuwa na taarifa za watoto ambao hakuwataja idadi kufariki, baada ya mama yao kuwapandisha juu ya kabati kwa lengo la kuwaokoa.

Hata hivyo, kabati hilo na nyumba walimokuwa ikiishi familia hiyo vilisombwa na maji huku mama wa watoto hao akikimbia kutafuta jia ya kujiokoa.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment