.

.

.

.

Thursday, December 01, 2011

SAKATA LA UNUNUZI WA RADA .........

SAKATA la ununuzi wa rada kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza limerudi kwa sura mpya baada ya Bunge la nchi hiyo kuitaka Serikali ya Tanzania iwafikishe mahakamani watu wote walioshiriki mchakato wa ununuzi wake na kuingiza nchi katika hasara ya mabilioni ya fedha.

Kupitia kamati yake ya Maendeleo ya Kimataifa, Bunge hilo limesema lingependa kuona watu wote walioshiriki kwenye mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi.

Taarifa ya kamati hiyo iliyonukuliwa jana na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), ilieleza kuwa wajumbe wake ambao ni wabunge kutoka vyama mbalimbali, watatoa ushirikiano wa dhati kwa Tanzania iwapo itaamua kuwashtaki watuhumiwa hao nchini Tanzania au Uingereza.

Wabunge hao walisema kuwa mbali na kurudishiwa fedha iliyozidi kwenye ununuzi huo, Tanzania inapaswa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote ili haki itendeke.

Wito huo wa wabunge wa Uingereza umekuja wakati tayari Kampuni ya BAE System, iliyoiuzia Tanzania rada hiyo, ikikubali kuwa kulikuwa na kasoro katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo na hivyo kuirudishia Tanzania Dola za Marekani 46 milioni kama fidia.

Hoseah adai mkanganyiko
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo jana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah alisema; "Kama Bunge la Uingereza linasema wafikishwe mahakamani na hukumu ilitolewa huko huko Uingereza, hapa kuna mkanganyiko."

Aliongeza: "Niko Tanga, sijapata taarifa, lakini ni vizuri ukasoma hukumu iliyotolewa Uingereza, ina ushahidi mwingi halafu tujadiliane kwenye hilo."

DPP: Tupeni ushahidi
Akizungumza na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Eliezer Feleshi alisema, "Kama Uingereza wana ushahidi, tuko tayari kwenda mahakamani hata kesho kwa sababu ofisi yangu inahitaji ushahidi ili iweze kupeleka kesi mahakamani."

Wito huo wa wabunge wa Uingereza umekuja miezi kadhaa tangu Serikali ya Tanzania itume wabunge wanne, wakiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai kwenda Uingereza kufuatilia suala la malipo ya fedha iliyozidi kwenye manunuzi hayo ya rada.

Wabunge wa Tanzania

Wabunge wengine walioambatana na Ndugai katika msafara huo ni Mussa Azzan, Angella Kairuki na John Cheyo.
Katika Mkutano wa Nne cha Bunge la Kumi, timu ya wabunge hao walioenda nchini Uingereza kufuatilia malipo ya rada kwa Serikali ya Tanzania ilikabidhi ripoti yake kwa Spika wa Bunge iliyopendekeza mambo mawili, ikiwamo kushtakiwa kwa wahusika wa sakata hilo hapa nchini.

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao waliwaeleza waandishi wa habari kuwa waligundua madhambi ya kutisha katika sakata la ununuzi wa rada hiyo ya kijeshi yanayoweza kuwatia hatiani wahusika.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment