.

.

.

.

Friday, January 13, 2012

UMEME BEI JUU !!!


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeidhinisha kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kuanzia jumapili hii Januari 15 mwaka huu.Ongezeko hilo halitawahusu wateja wa hali ya chini, wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), huku wafanyakazi wa shirika hilo wakitakiwa kulipa gharama za umeme kama watumiaji wengine.

Katika bei hizo, wateja wa hali ya chini wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi,  bei itabaki kuwa Sh 60 kwa uniti wakati watumiaji wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 50, bei hiyo itapanda kutoka Sh 195 hadi kufikia Sh 273 kwa uniti.
Watumiaji wa kawaida wakiwemo wenye biashara ndogondogo, bei imepanda kutoka Sh 157 hadi Sh 221 kwa uniti wakati watumiaji umeme mkubwa wa kati, bei imepanda kutoka Sh 94 hadi Sh 132 kwa uniti, wakati watumiaji umeme mkubwa hasa wenye viwanda na migodi, bei imepanda kutoka Sh 84 hadi Sh 118 kwa uniti na kwamba Zeco wamepandishiwa kwa asilimia 28.21 kutoka awali ambako, walikuwa wakilipa Sh 83 na sasa watalipa Sh 106 kwa uniti.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema bei hizo hazihusishi kodi na kwamba Tanesco walitaka umeme upande kwa asilimia 155 lakini, baada ya mamlaka hiyo kuchambua maoni ya wadau, iliamua upande kwa asilimia 40.29 ili maisha yasizidi kuwa magumu.

Masebu alisema ongezeko hilo ambalo ni la dharura, litadumu kwa muda wa miezi sita na kwamba baada ya hapo, Ewura itafanya tathmini nyingine ya  kujiridhisha juu ya huduma zinazotolewa na Tanesco na matokeo yake yanaweza kupandisha au kushusha gharama ya umeme.

No comments:

Post a Comment