MSUGUANO kati ya wabunge wa Dar es Salaam na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, umeibuka upya baada ya wabunge hao kusema wamepata nyaraka mpya za tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria katika suala la ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Kamati ya Wabunge hao waliokutana jana kwa dharura kujadili nyaraka hizo, imepanga kutoa taarifa kuhusu uamuzi na maazimio ya kikao na hatua ambazo watachukua leo. Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Kamati hiyo, John Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, ilisema walikutana kwa dharura chini ya uenyekiti wa Abbas Mtemvu, Mbunge wa Temeke. “Wabunge wa Dar es Salaam wanaendelea na kikao cha kupitia nyaraka zote na kufanya uamuzi wa hatua za kuchukua na taarifa juu ya hatua hizo itatolewa kwa umma baada ya kumalizika kwa mkutano unaoendelea,” Mnyika alisema jana. Wabunge walioshiriki mkutano huo ni Mtemvu (Mwenyekiti), Mnyika (Katibu), Halima Mdee, Mussa Zungu, Idd Azzan, Neema Mgaya Hamid, Suzan Lyimo, Zarina Madabida, Faustine Ndugulile, Phillipa Mturano na Eugene Mwaiposa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyaraka ambazo Kamati hiyo imepokea ni pamoja na barua ya UDA ya Januari 26 yenye kumbukumbu namba CBA/Reg/01/UDA ambayo inataka dola za Marekani 133,125 zitolewe kutoka akaunti ya UDA ambayo ilishaagizwa awali fedha zisitoke kinyemela. Waraka mwingine uliojadiliwa ni wa kikao kinachodaiwa kuwa cha wanahisa wa UDA cha Februari 13 ambacho inadaiwa kilifanywa na Meya Masaburi akiwa Mwenyekiti pamoja na Robert Kisena ambaye anatambulishwa kwenye muhtasari huo kama Mwenyekiti Mtendaji wa UDA na Katibu wa Bodi ya UDA. Wabunge hao wanakishutumu kikao hicho pamoja na mambo mengine, kuwa kimefanya uamuzi haramu wa kubadili waweka saini katika akaunti ya UDA iliyozuiwa kwa lengo la kuwezesha fedha kutolewa kinyemela na Simon Group. Wanadai kwamba Meya Masaburi kwa kushirikiana na Simon Group wameshirikiana kwa mara nyingine kukiuka uamuzi wa mamlaka mbalimbali na sheria na kanuni. Kwa mujibu wa wabunge hao, Januari 9, Baraza la Madiwani wa Jiji lilipitisha maazimio kuhusu mgogoro unaoendelea katika UDA mojawapo ikiwa ni pamoja na kufanyika uchunguzi wa kughushiwa kwa barua iliyomwelekeza Simon Group Limited kulipa awamu ya pili ya malipo kwa kutumia akaunti ya Mwenyekiti wa Bodi ya UDA na kwamba suala lipelekwe kwenye vyombo husika kwa ajili ya kubaini ukweli na hatua kali zichukuliwe dhidi ya aliyeghushi. Taarifa hiyo iliongeza, kwamba Baraza la Madiwani liliazimia kuwa uthamini wa hisa uliotumiwa katika kumwuzia hisa Simon Group, haukuwa halisi hivyo hisa zote zifanyiwe uthamini upya ili ziuzwe kwa bei inayostahili. Ilielezwa pia kuwa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, liliazimia kuwa Simon Group asitambuliwe kama mwanahisa mkuu katika UDA na hivyo kuazimia kuwa iteuliwe Bodi ya muda itakayosimamia utekelezaji wa mkataba kati ya UDA na Simon Group. Taarifa iliendelea kueleza, kwamba Baraza lilimteua Mwaiposa kuwa mjumbe wa Bodi hiyo akiwakilisha Halmashauri ya Jiji na Meya Masaburi kinyume na maazimio ya mkutano wa Januari 9, akashiriki kikao cha Bodi ya UDA Februari 13 na kudaiwa kufanya uamuzi wa kubadili waweka saini wa akaunti ili fedha zihamishwe. Agosti 4 mwaka jana, wabunge wa Dar es Salaam walikutana Dodoma na kutoa tamko la kueleza kile walichosema ni kusikitishwa na tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa UDA. Tuhuma za wabunge hao kwa Masaburi ziliibuka mwaka jana ambapo Meya huyo alilazimika kutumia kauli kali baada ya wabunge hao kumtaka ajiuzulu kupisha uchunguzi akisema wabunge hao baadhi yao wanashindwa kufikiri kwa kutumia vichwa na badala yake wanatumia makalio. |
.
.
Wednesday, February 29, 2012
SUALA LA UFISADI UDA LAIBUKA UPYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment