.

.

.

.

Wednesday, March 28, 2012

HILI NDILO TATIZO LA TANESCO

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), linadaiwa sh. bilioni 269 na Kampuni ya Kufua Umeme ya Aggreko ikiwa ndio sababu ya shirika hilo, kushindwa kutoa huduma ya umeme kwa ufanisi. Kutokana na deni hilo, Kampuni ya Aggreko imelazimika kuzima mitambo yake baada ya kukosa fedha za kununulia mafuta yanayotumika kuendeshea mitambo. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Bw. January Makamba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Bw. Makamba alisema, Serikali iliombwa kuikopesha TANESCO sh. bilioni 408, lakini fedha hizo hadi sasa hazijatolewa ili kusaidia kulipa deni hilo. “Hata kama TANESCO watapewa hizi fedha, kwanza tunapaswa kulipa deni la sh. bilioni 269 na kiasi ambacho kitabaki hakitoshelezi kununua mafuta ya kuendeshea mitambo hii,” alisema. Alisema Kampuni ya Aggreko ilizima mitambo yake tangu Desemba 2011 kwa sababu ya kukosa fedha za kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo. “Kimsingi tatizo la mgawo wa umeme litarrudi kama zamani kutokana na vyanzo vya maji ambavyo vinatumika kuzalisha umeme kupungua, kwa sasa umeme tunaopata unatokana na vyanzo hivi. “Maji yaliyopo kwenye mabwawa ni kidogo, ikifika Agosti mwaka huu itakuwa kipindi cha kiangazi sasa hali itakuwa mbaya zaidi, njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kuharakisha ujenzi wa bomba la gesi ambalo Rais Jakaya Kikwete alitoa tamko lijengwe kwa miezi 18 tangu 2011,” alisema Bw. Makamba. Alisema kukamilika kwa bomba hilo, kutaondoa mgawo kwani umeme wa uhakika utakuwa ukipatikana muda wote. “Kama tutaendelea kuzalisha umeme kwa kutegemea mafuta, nchi yetu itaelekea kubaya kwani gharama za mafuta zinaongezeka siku hadi siku,” alisema. Kuhusu utaratibu mpya wa kuagiza mafuta kwa pamoja ambao umeanzishwa hivi karibuni kwa Sheria ya Bunge, Bw. Makamba alisema haujasaidia kupunguza bei ya nishati kama ilivyotarajiwa. Akizungumza na wadau wa mafuta, Bw. Makamba alisema hivi sasa kamati yake itakaa na kupitia upya kanuni na sheria ili kuangalia njia mbadala za kupunguza bei ya nishati hiyo kama ilivyokusudiwa. Alisema kati ya kampuni zilizokubaliwa kununua mafuta kwa pamoja, hadi sasa zabuni mbili zimeagizwa na mara ya kwanza ilikuwa Januari na Februari. Aliongeza kuwa, kipindi hicho ziliingia meli 16 zenye shehena ya mafuta ambapo awamu ya pili ilikuwa iwe Machi na Aprili mwaka huu kwa kuingia meli 17 lakini hadi sasa zimeingia meli mbili tu. Bw. Makamba alisema meli zimekuwa zikichelewa tofauti na walivyokubaliana kuwa zitaingia zote ambapo changamoto iliyopo ni bei ambayo haijashuka. Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Masoko kutoka Shirika la Maedeleo ya Petroli nchini (TPDC), Bw. Leo Lyayuke, alisema hivi sasa wanakabiliwa na changamoto nne. Changamoto hizo ni kampuni za kuagiza mafuta, upatikanaji wa zabuni, ongezeko la bei na uchelewaji wa meli. Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Godwin Samuel, alisema imebainika baadhi ya mafuta yanayoingizwa nchini hasa petroli hayana ubora wa kutosha. Alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa wanachukua sampuli ya mafuta yanayobaki bandarini na kuyapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini yana matatizo gani

No comments:

Post a Comment