.

.

.

.

Tuesday, March 20, 2012

MH.MWAKYEMBE AANZA KAZI OFISINI

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe, amerejea rasmi ofisini na kuanza kazi huku akivitaka vyombo vya habari nchini kuachana na suala la ugonjwa wake, akisema sasa imetosha. Waziri huyo alikaa nje ya ofisi kwa takribani miezi mitano baada ya kuugua ugonjwa wa ngozi unaodaiwa kupukutisha ngozi yake na kukimbizwa India kwa matibabu. Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuingia ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe alisema hali yake sasa inaendelea vizuri na ndiyo maana amerejea kazini. “Naomba nitumie fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa nilikuwa naumwa kwa muda mrefu ugonjwa uliojulikana kitaalamu baada ya vipimo kama Populia Thrulema yaani matatizo ya ngozi, lakini sasa naendelea vizuri,” alisema Dk. Mwakyembe ambaye alionekana mchangamfu huku akiwa bila glovu mikononi kama ilivyozoeleka tangu aanze kuugua. Awali akiwasili eneo la ofisi za Wizara ya Ujenzi, alikutana na kundi la waandishi wa habari hali iliyomfanya ashuke haraka kwenye gari na kuingia ndani kwa mwendo wa kasi sana, huku akiishia kuwasalimia waandishi hao na kupanda ngazi akikimbia. Alirejea nchini Jumamosi kutoka India. Hata hivyo, baadaye alipozungumza na waandishi hao, aliviomba vyombo vya habari vipumzike kuandika na kuchokonoa kuhusu ugonjwa wake na badala yake waiachie Serikali ambayo imeunda tume kuchunguza chanzo cha ugonjwa huo, ikamilishe uchunguzi wake. “Naomba jamani sasa ugonjwa wa Mwakyembe ufike mwisho kuandikwa. Watu walitarajia na kusubiri mengine, lakini nawaambia mliotaka kuandika vichwa vya habari vya kifo changu mjue tafadhali niko hapa sijafa, naomba yaishe sasa,” alisema Dk. Mwakyembe. Alisema alipokuwa India kwa mara ya pili kuendelea na matibabu, alitaarifiwa kuwa suala la utata wa ugonjwa wake kuwa ama amelishwa sumu au la, limeundiwa timu na Serikali ambayo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na polisi wamo ndani yake. Alisema sasa suala hilo anamwachia Mungu na Serikali inayolichunguza, ambapo alikataa kuzungumzia zaidi kwa nini anahisi alilishwa sumu. “Hili mnalolihoji nitalizungumza kwenye timu hiyo itakayokuja kunihoji, nawashauri muwe na subira ikikamilisha uchunguzi wake, itasema na hata mimi nitasema.”

No comments:

Post a Comment