.

.

.

.

Tuesday, March 13, 2012

QATAR AIR KUANZA KUTUA KIA

NDEGE za Shirika la Qatar zinatarajiwa kuanza safari kati ya Doha na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuanzia Julai mwaka huu. Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Akbar Al Baker alitoa taarifa hiyo wakati wa maonesho makubwa ya wakala wa usafirishaji wa anga na utalii maarufu kama ITB Berlin, yaliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita Jijini Berlin, Ujerumani. Alisema, shirika hilo itatoa huduma za anga uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro ikitumia ndege aina ya Airbus A320 kupitia jiji la Nairobi. Mkurugenzi Mtendaji wa KIA, Marco van de Kreeke alisema kuanzisha kwa safari hiyo kutafungua milango kwa wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati, India, China na nchi nyinginezo za Asia. Alisema, wanatarajia huduma mpya za kila siku kupitia Doha zitasaidia kukua na kurahisisha uwanja wa ndege wa Kilimanjaro kuchangia uchumi wa taifa na kutangaza vivutio vilivyopo Kaskazini. Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dk Aloyce Nzuki akitoa maelezo juu ya umuhimu wa safari hiyo katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini, alisema mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani ikiwemo Tanga, Arusha na Manyara itafaidika kupitia vivutio vya kitalii na baadaye kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini. Taarifa ya ujio wa ndege za shirika la Qatar imekuja baada kutangazwa kwa ukarabati wa uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro utakaogharimu dola za kimarekani milioni 35 . Mradi huo ulioanza tangu Januari mwaka jana utajumuisha marekebisho ya njia za ndege mpya ili kuuongezea uwezo uwanja na upanuzi wa majengo yanaozunguka uwanja . Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro mpaka sasa unatoa huduma kwa abiria 650,000 kwa mwaka. Idadi ya wasafiri kutoka nje imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 15 kila mwaka kutoka 2003. Shirika la Ndege la Qatar linafanya safari mbalimbali duniani kutumia ndege za kisasa 105 na kuunganisha vituo 112 vya kibiashara na mapunziko barani Ulaya, Mashariki ya Kati, Afrika, Asia, Pasifiki, Amerika ya Kaskazini na ya Kusini.

No comments:

Post a Comment