MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh jana aliwasilisha ripoti yake bungeni inayoonyesha kuendelea kuwapo kwa ufisadi wa kutisha serikalini huku deni la taifa likiongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka juzi na kufikia Sh14.4 trilioni mwaka jana.
CAG alisema Serikali imetumia Sh 544 bilioni bila kuidhinishwa na Bunge, Sh bilioni moja zimelipwa mishahara kwa watumishi hewa na Sh 3bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi ambazo ziko nje ya bajeti iliyoidhinishwa na mhimili huo wa dola wa kuisimamia Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Utouh alisema deni la taifa limeongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka wa fedha wa 2009/2010 hadi kufikia Sh14.4 trilioni mwaka 2010/2011, sawa na ongezeko la asilimia 38.
“Kuna ongezeko kubwa la deni la taifa, lakini hoja hapa si kuongezeka kwa deni la taifa bali ni kwamba deni hili limeletwa kwa mikopo yenye manufaa kwa taifa na yenye kukuza uchumi wa nchi? Hii ndio hoja ya msingi ya kuangalia,”alisema.
Ufisadi balozi na Mfuko wa Jimbo
Kuhusu ukaguzi katika balozi zote 32, Utouh, alisema ukaguzi uliofanywa katika ofisi hizo umebaini kuwapo matumizi yasiyoridhisha na kuwapo kwa Sh3 bilioni ambazo zimetumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri.
Kuhusu Mfuko wa Jimbo (CDCF) ulioanzishwa kwa Sheria ya Bunge, ripoti hiyo inaonyesha kuwa Sh2.6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za mfuko huo hazikutumika katika Halmashauri 51 zilizokaguliwa.
Kwa upande wa mashirika ya umma, alisema baadhi yake hayana bodi za wakurugenzi, vikao vya bodi haviitishwi kwa wakati na baadhi ya mashirika hayo huchelewa kukamilisha hesabu zao za mwaka kwa wakati.
Misamaha ya kodi na mfumo bajeti
Mbali na kukua huko kwa deni la taifa, CAG alisema pamoja na wananchi, wabunge na asasi za kiraia kupigia kelele misamaha ya kodi, ukaguzi umeonyesha kuwapo kwa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.02 trilioni.
Alifafanua kuwa taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilionyesha kuwa misamaha ilitolewa kwa taasisi mbalimbali yenye thamani ya Sh1,016,320,300,000 ambazo ni sawa na asilimia 18 ya makusanyo yote nchini.
Kwa mujibu wa Utouh, kama kiasi hicho kisingesamehewa, TRA ingekusanya Sh6.5 trilioni ikiwa ni sawa na Sh717.4 bilioni zaidi ya kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ambacho ni Sh6,566,525,544,378.
“Siku zote tumekuwa tukipiga kelele kuhusu misamaha ya kodi ingawa tunasema misamaha ya kodi haiepukiki, lakini lazima isimamiwe na iwe ni lazima kutolewa…kwa kweli eneo la misamaha ya kodi ni la kutazamwa,”alisema.
Alikosoa mfumo mzima wa mchakato wa kupitisha bajeti akisema, mjadala wa bajeti huanza Juni hadi Agosti kila mwaka wakati sheria ya matumizi ya fedha zinazopitishwa hutakiwa kuanza Julai mosi.
Alifafanua kwamba mjadala wa bajeti huanza kwa kujadili bajeti ya taifa ambayo pia hupitishwa kabla ya kuanza kujadili fungu moja moja la bajeti na hivyo, kufanya mchakato mzima wa kupitisha bajeti uonekane ni kugonga tu mhuri.
“Utaratibu huu unafanya mchakato mzima wa bajeti uonekane kama ni zoezi la rubber stamp (kugonga mhuri) kwani wabunge tayari walishapitisha bajeti ya taifa ambayo kimsingi inatokana na bajeti za fungu moja moja,” alisema.
CAG alipendekeza Serikali ijadiliane na Bunge kuhusu uwezekano wa kubadili mzunguko wa bajeti ya taifa ili kuruhusu mabadiliko ya tarehe za majadiliano kukamilika, kabla ya au ifikapo Juni 30 ya kila mwaka.
Katika mapendekezo hayo, CAG alisema mjadala wa wabunge kuhusu bajeti uanze kwa kujadili bajeti za fungu moja moja na bajeti ya taifa iwe ya mwisho kujadiliwa ili kuondoa ile dhana ya kuwa na bajeti isiyo na uhalisia.
Hali katika halmashauri
Alisema kuwa ukaguzi maalumu uliofanywa katika halmashauri za wilaya za Sengerema, Ludewa, Kishapu, Kilindi, Moshi,Monduli, Longido na Manispaa ya Ilala umebaini kuwapo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
CAG pia aliagiza kufanywa ukaguzi maalumu katika Halmashauri za Arusha, Songea, Morogoro, Kilindi na Misungwi kutokana na kutoridhishwa na taarifa za Halmashauri hizo kuhusu matumizi ya fedha za umma.
Akizungumzia ufisadi huo mara baada ya taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Augustino Mrema, alisema bado CAG ana kibarua kigumu kutokana na kuwepo mtandao wa mafisadi ndani ya halmashauri.
“Kwa ripoti hii ya CAG nchi inadidimia, nchi inasambaratika ni kama tunafanya mchezo wa kuigiza mimi napendekeza kiundwe kikosi kazi maalumu cha kupambana na mtandao wa wizi ndani ya halmashauri nyingi nchini," alisema Mrema
Alisisitiza kuwa nchi imezidiwa nguvu na wezi na mafisadi ndani ya halmashauri, ambao wamejipanga kila kona kutekeleza wizi wao kwa kuwa haiwezekani kila mwaka kuwepo ripoti za ubadhirifu wa mabilioni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, alisema CAG ametimiza wajibu wake kikatiba na sasa ni kazi ya wabunge kuhakikisha Bunge linatoka na maazimio juu ya ripoti hiyo.
Mbali na Zitto, kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu(PAC), John Cheyo alionyesha kushangazwa na kuendelea kukua kwa deni la taifa wakati miradi mingi nchini haina fedha.
“Deni la taifa linatupa matatizo sisi wote hapa kwa sababu mimi sielewi maana tunakopa, lakini miradi yetu haina pesa hapa kuna kitendawili,”alisema Cheyo na kusema Bunge itabidi lijadili na kutegua kitendawili hicho.
Katika hatua nyingine, CAG Utouh amesema Ripoti ya Ukaguzi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), tayari imekamilika na amekwishaikabidhi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda tangu Aprili 6 mwaka huu.
Agosti 13 mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Mkuchika alikambidhi CAG kazi ya ukaguzi wa hesabu za UDA na mchakato wa uuzwaji wa hisa zake ambao unahusisha vigogo mbalimbali akiwemo, Idd Simba.
Akizungumza jijini Dares Salaam juzi, CAG Utouh alisema tayari ripoti iko kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya hatua zaidi.
Alisema Aprili 6 mwaka huu baada ya kukamilika kwa ukaguzi, aliikabidhi kwa Waziri Mkuu kufuatia kukamilika kwa ukaguzi wa ripoti hiyo.
“Kwa sasa mimi nimeshamaliza kazi yangu ya ukaguzi wa UDA, ambapo Aprili 6 mwaka huu siku ya Ijumaa kuu, ndipo nilipo ikabidhi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda,” alisema Utouh na kuongeza;
“Kitu ambacho kinatakiwa sasa ni kusubiri ripoti hiyo ipitiwe na Waziri Mkuu ndipo taarifa rasmi nini kilichokaguliwa na kilicho patikana katika ripoti hiyo kitawekwa wazi,” alisema.
CAG,alibainisha kwamba kwa sasa yeye kama mtu aliyepewa jukumu la kufanya kazi hiyo ya ukaguzi, amesha ikamilisha kwa kila kitu na kwamba ripoti hiyo haipo tena mikononi mwake.
“Ndugu zangu kwa sasa mimi sina tena hiyo ripoti ya UDA na kwamba kitu kinachotakiwa sasa ni kuwa wavumilivu kwani baada ya muda mfupi Waziri Mkuu akiipitia, kila kitu kitawekwa wazi,” aliseama.
Hatua hiyo inafuatia kuibuliwa kwa kashfa ya uuzaji UDA na wabunge wa Dar es Salaam Agosti mwaka jana kwamba, taratibu zilikiukwa wakati wa uuzaji dhidi ya Kampuni ya Simon Group, inayomilikiwa na Robert Kisena.
Baadhi ya vigogo wanaodaiwa kuhusika na kashfa hiyo, ni Meya wa Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, Idd Simba, na Meneja Mkuu wa UDA, Victor Milanzi. Wote wamehojiwa na tume.
UDA ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja na Halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu kupitia Hazina, wakiwa na jumla ya hisa milioni 15, kila hisa moja ikiwa na thamani ya Sh100.
Kutokana na mchanganuo huo, Halmashauri ya Dar es Salaam ilikuwa inamiliki asilimia 51 ya hisa hizo, huku Hazina ikimiliki asilimia 49.
Februari 11, mwaka jana, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA, chini ya Idd Simba, ilikutana na uongozi wa Simon Group ikiongozwa na Kisena na kusaini mkataba, ambao ulithibitisha kwamba UDA ilikuwa imeiuzia Simon hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.535 ya hisa zote kwa thamani ya Sh1.142 bilioni.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment