.

.

.

.

Thursday, January 10, 2013

PRECISION AIR KUANZA SAFARI ZA MBEYA


SHIRIKA la Ndege la Precision Air linatarajia kuzindua safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kuanzia Ijumaa ijayo.
Hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uhusiano, Linda Chiza alisema abiria wa safari hiyo, watahudumiwa na ndege aina ya ATR-72, yenye uwezo wa kubeba abiria 70.
Alisema kwa mujibu wa ratiba ya shirika, ndege hiyo itakuwa inaruka mara nne kwa wiki kwenda Mbeya na kwamba safari hizo zitaongezeka kwa kadri njia hiyo itakavyoimarika.
“Lengo ni kuwapa abiria wetu unafuu wa kuchagua muda wa kusafiri unaowafaa kulingana na ratiba zao,” alisema Linda.
“Tunajivunia kuzindua safari hii mpya kuelekea Mbeya ambayo itatuwezesha sasa kuwapatia huduma abiria kutoka Mbeya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.  Alielezea matumaini ya shirika lake kuwa kwa kupeleka huduma hizo mkoani Mbeya, litakuwa  linarahisisha usafiri kwa watalii, wafanyabiashara na  watu wengine wanaopenda kutembelea mkoa huo wenye utajiri wa vivutio vya utalii.
Vivutio hivyo ni pamoja na  Mbuga ya Taifa ya Wanyama ya Ruaha na Katavi na Hifadhi nyingine nyingi za taifa.
“Tunatambua pia kuwa Mkoa wa Mbeya ni lango la kibiashara kwa nchi jirani za Zambia na Malawi, hivyo kuufanya kuwa mkoa wa kibiashara,” alisema Linda.
Alisema uzinduzi wa safari ya Mbeya unafikisha idadi ya maeneo yanayohudumiwa na shirika hilo hapa nchini, kufikia 18 na kulifanya shirika hilo kuwa shirika la ndege kubwa kuliko yote nchini.
Aliwahakikishia wateja wa shirika hilo kuwa kampuni yake itaendelea kutoa huduma za usafiri wa anga za kipekee na  za uhakika.

No comments:

Post a Comment