.

.

.

.

Saturday, February 09, 2013

SHUKURANI ZA DHATI TOKA KWA KATIBU WA CCM UINGEREZA KWA MH.RAIS
Naomba kuchukua fursa hii kutoa shukrani za dhati na wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete na Serikali yake ya awamu ya nne, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba yaTawi la CCM UK na nina imani kwa niaba ya wana jamii ya Wa-Tanzania Walioko Nje ya Nchi (Dispora)  kwa Ujumla, katika juhudi anazofanya kujumuisha Dispora Tanzania kwenye kuchangia maendeleao ya Nchi yetu.

Wana-Dispora tulio wengi tumeshuhudia kwa vitendo
tangu Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake imeingia Madarakani , jitihada  na mikakati tofauti na iliyo wazi  ya Serikali Kuu  kutafuta mbinu za kudumu ili kushirikiana na kuwahusisha wana Diaspora, katika kuchangia maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii ya Nyumbani, Tanzania.

Nakumbuka Mheshimiwa Rais Kikwete katika kikao chake cha kwanza na Watanzania waishio Uingereza Mnamo mwaka wa fedha 2006/2007  pale Churchill Hotel, UK , katika Hotuba yake ambayo mbali na kutuelezea mafanikio na mikakati mbalimbali iliyopangwa na serikali yake kwenye utekelezaji wa Sera zake za Serikali ya awamu ya nne, kwa nia ya  kutimiza maazimio ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2005 na baadae 2010, vile vile alituahidi wana-Dispora kuwa atahakikisha yeye Binafsi atafanya jitihada zake zote kwa kadri ya uwezo wake aliyopewa na Mwenyezi Mungu  na Serikali yake haitusahau na katuacha nyuma Wana-Dispora . Kilichoendelea baada ya Mkutano ule wana Dispora UK tulishudia thamani yetu kwa Serikali na Taifa letu ,kwani tumekuwa tukipewa kipaumbele kwa kila Kiongozi Mkuu wakiwemo Mawaziri na Wabunge wetu tofauti,  wanapotembelea  Uingereza (na nina imani Nchi nyingine mbalimbali ) mbali na kuwa na ratiba zao ndefu za  kikazi, wanapata  muda wa kubadilishana mawazo nasi na tunaona matunda ya mchango wetu yameanza kuonekana ,licha ya kuwepo changamoto za kawaida zinazokabilika.  Hili  tunamshukuru sana Rais wetu kwa kulipa uzito unaostahili na kuonyesha mfano wa Uongozi wake bora na uliotukuka.

Kwa mara ya kwanza Tanzania Dispora  tumepata sauti na kuthaminiwa kwa wazi kwa Mchango wetu wa hali na  mali tunaorudisha nyumbani ili kuchangia Maendeleo ya Nchi. Wana-Dispora sasa  tunajivunia kupewa  na  Rais wetu  jina la Mkoa . Baada ya kuanza na dawati la Dispora pale Wizara ya Mambo ya Nje, ili kuweka mfumo wa kudumu na kutimiza ahadi yake Mheshimiwa Rais mwaka ulipita 2012 aliteua Mkurugenzi wa Idara ya Dispora. Sasa tuna Idara/Kitengo kizima na si dawati tena. Kitengo/Idara yenye jukumu la kushughulikia mambo muhimu na tofauti ya Dispora. Hii ni hatua kubwa sana na ya muhimu na hatutaacha kumshukuru Rais wetu kwa kuliona na kulitambua hili na kutuletea matunda yake.

Licha ya yote hayo ya kiutendaji yanayoendelea, na jambo kubwa lililofanya kuandika shukrani hizi za dhati na za wazi ni kilichotendeka wiki iliyopita kupitia vyombo vya habari na Blogu za jamii tumeshuhudia tukio la kihistoria pale ambapo Rais Jakaya Kikwete, Chini ya Ofisi yake Ikulu , wametoa fursa kwa Wa-Tanzania Wataalamu waliopo Nje na Ndani ya Nchi kupeleka  wasifu wao (CV) moja kwa moja Ofisi za Katibu Mkuu Kiongozi -Ikulu,   ili tuweze kupata nafasi za kazi kuchangia moja kwa moja na kuwa mstari wa mbele kuijenga nchi yetu . Hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha Watanzania (na hususan Wana-Dispora) kuomba serikali kutumia zaidi wataalamu wa kitanzania na si wa kigeni , na  tumefurahi sana kuwa Serikali yetu kwa mara ya kwanza na kwa uwazi kabisa  imetusikiliza kwa hili .

Naomba kutoa wito na shime kwa WaTanzania wote waliopo nchi mbalimbali  duniani  , ni wakati umefika sasa Nchi yetu inatuhitaji na Serikali yetu imetupa nafasi hii adhimu basi na tujipange na tujitokeze kwa wingi ili tuweze kwenda nyumbani kuchangia maendeleo ya Tanzania yetu katika nyanja tofauti na kwa kadri ya uwezo wetu na kwa yale mazuri tuliyojifunza Ughaibuni. 

 naomba kumalizia kwa ule usemi usemao kuwa "Asiyemshukuru Binadamu mwenzie basi hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru " na kwa mantiki hiyo, kwa heshima kubwa Naomba kutanguliza shukrani zangu za dhati  kwa mpendwa Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete kwa kujitolea kwake na kufanya kazi ngumu mno ya kuliongoza Taifa letu na nakumuombea kwa Mwenyezi Mungu yeye  Binafsi na Viongozi wetu wote afya njema na hekima za kuweza kupambana na majukumu yao ya kila siku .

Kwa Wana -Dispora Wenzangu popote pale mlipo Duniani , ngoma iko uwanjani na tuicheze sasa, CV zinahitajika .........haya mama  Harambeeeee

Mugu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

Umoja Ni Ushindi .

Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

Mariam Mungula
Katibu wa CCM - Uingereza 

No comments:

Post a Comment