.

.

.

.

Thursday, July 25, 2013

UFISADI ..........................

 Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ichunguze kashfa ya matumizi tata ya Sh8 bilioni zilizotumika wakati wa Mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliohusisha viongozi kadhaa wa Afrika ambao ulifanyika nchini hivi karibuni.
Akifungua mkutano wa siku tatu wa Baraza la Vijana la Katiba Tanzania Dar es Salaam jana, Waziri Sitta alidai kwamba fedha hizo zimefujwa na baadhi ya watumishi wa Serikali ambao walijitengenezea kampuni bandia ambazo hazijasajiliwa.
“Shilingi bilioni nane zimekwenda kutokana na kampuni hewa baada ya Rais kuwakaribisha wageni nchini hivi karibuni.... kisa Rais kapata wageni watu wametengeneza kampuni hewa za mapambo, machapisho na fedha zimeliwa,” alisema Sitta na kuongeza: “Hivi sasa uchunguzi unaendelea, lakini hatuwezi kuwa kila siku ni uchunguzi tu na wakati mwingine uchunguzi umekuwa hauna matokeo.”
Alisema watumishi kama hao hawafai kwa kuwa wanatumia nafasi muhimu kwa nchi kujinufaisha wao binafsi.
Mkutano wa Smart Partnership Dialogue ulifanyika Dar es Salaam kuanzia Juni 28 hadi Julai Mosi mwaka huu.
Alisema walifahamu kuhusu ufisadi huo baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kueleza kuwa kuna utata kwenye fedha hizo na kwamba kampuni tatu hewa zililipwa fedha wakati hazijasajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
“Kuna kampuni kama tatu, hizi nasikia zimeshachukuliwa hatua kwa kuwa ni hewa lakini bado... lazima CAG afanye ukaguzi kwa hizo Sh8 bilioni,” alisema Sitta.
Sitta ambaye amekuwa akijipambanua kuwa ni mmoja wa kundi la viongozi wanaopinga ufisadi, alisema watumishi wa jinsi hiyo, hawafai kwa kuwa wanatumia nafasi muhimu kwa nchi kujinufaisha binafsi.
“Pamoja na yote, kampuni zina watu, lazima na wao wachukuliwe hatua. Wahusika wote ninaamini wanafahamika sasa isifikie hatua tunaambiwa uchunguzi usiofikia mwisho,” alisema Sitta.
Hata hivyo, Balozi Sefue hakupatikana jana kuelezea tuhuma hizo ambazo hivi karibuni ziliripotiwa na gazeti moja la kila wiki kwani simu yake iliita bila ya majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu na baadaye simu yake haikuwa tena hewani

No comments:

Post a Comment