Mwasiti Suleiman (kulia) akiwa na waimbaji wenzake wa TOT katika moja ya maonyesho ya kikundi hicho.
MWIMBAJI Mwasiti Suleiman wa kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT Plus) ameamua kujiengua katika kikundi hicho.
Mwasiti amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa, ameamua kujiengua TOT Plus kwa sababu ya maslahi duni.
Amesema amekuwa akifanyakazi katika kikundi hicho kwa zaidi ya miaka tisa na kuongeza kuwa, hakuwahi kuajiriwa zaidi ya kufanyakazi kama kibarua.
Amesema katika miaka miwili ya kwanza, hakuwa akilipwa chochote na kwamba katika miaka saba iliyofuata, alikuwa akilipwa posho.
Mwasiti amesema kwa sasa ameamua kufanyakazi katika kampuni moja ya Wakorea, ambayo hakutaka kuitaja, lakini pia amekuwa akijihusisha na muziki huo katika vikundi vya mitaani.
Mwanadada huyo amesema haoni tofauti yoyote katika maisha yake ya sasa na wakati alipokuwa akifanyakazi TOT Plus na kwamba muziki haikuwa ajira pekee ya kuendesha maisha yake.
"Nilipo naweza hata kuuza vitumbua au maandazi kwa sababu zote ni kazi. Kila siku tunapishana na akina mama wakifanyakazi mbalimbali na wanaishi,"amesema mwanamama huyo mwenye mwanya wa kuvutia.
Alisema hakuwahi kugombana na mtu yoyote kwa kipindi chote alichokuwa TOT Plus na kwamba aliwaaga viongozi wake huku akiwaeleza wazi kwamba maslahi duni ndiyo yaliyomkimbiza.
Amesema anaweza kuwa tayari kurudi katika kikundi hicho iwapo tu atahakikishiwa ajira na maslahi mazuri.
Mwanadada huyo amesema pia kuwa, yupo tayari kujiunga na kikundi kingine cha taarab iwapo kitamuhakikishia ajira na maslahi mazuri.
No comments:
Post a Comment