.

.

.

.

Saturday, June 13, 2015

TUZO ZA KTMA KUSHINDANIWA USIKU HUU

Kitendawili cha muda mrefu cha ‘nani mbabe kati ya Ali Kiba na Diamond’ huenda kikapata moja ya majawabu yake leo usiku, wakati wa tamasha la Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (KTMA) zitakazofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Wasanii hao wanapambana katika tuzo saba, ingawa Diamond anaonekana kuwa na nafasi zaidi ya kumuacha Ali Kiba kutokana na kutajwa kwenye tuzo 10 na hivyo kuwa na nafasi ya kufikia tena rekodi yake ya kuzoa tuzo nyingi kama mwaka jana.
Bendi ya muziki wa dansi ya Mashujaa pia iliwahi kunyakua tuzo tano mwaka 2013 lakini bado hakuna aliyewahi kumfikia 20 Percent aliyefanya kufuru mwaka 2011.
Washindi wa tuzo hizo wanatokana na kura zilizopigwa na mashabiki kwa njia ya sms, ingawa mara nyingi hutokea manung’uniko baada ya washindi kutangazwa kutokana na kuwapo hisia za upendeleo.
Bado ni kitendawili kigumu kwani asilimia kubwa ya wasanii wanawania tuzo zisizozidi sita kila mmoja, isipokuwa Ali Kiba, anayewania tuzo nane na Diamond Platnumz anayewania tuzo 10. Wawili hao pia wanapambana na wasanii wengine kwenye tuzo kama Mtumbuizaji Bora wa Mwaka wa Kiume ambayo inashindaniwa pia na Mzee Yusuf na Christian Bella.
Nyota hao pia wanapambana kwenye tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka, Mwimbaji Bora wa Kiume, Wimbo Bora wa Afro Pop, Wimbo Bora wa Zouk, Mtunzi Bora, Mtumbuizaji Bora wa Mwaka na Video Bora ya Mwaka ambayo kwa kawaida huenda kwa mtayarishaji.
Ingawa Diamond Platinumz amekuwa na mafanikio makubwa kimataifa hasa kutokana na kibao chake cha “Number One” alichofanya remix na wasanii wa Nigeria, anakabiliwa na upinzani mkali nyumbani kutokana na kuibuka upya kwa Ali Kiba, ambaye wimbo wake wa “Mwana” umetajwa kwenye tuzo nyingi. Ushindani wao katika sanaa umesababisha mijadala mikubwa miongoni mwa mashabiki wao, kiasi cha kufanya tamasha la leo kuwa moja ya vipimo vitaklavyowawezesha kujua nani ni mkali baina yao.
Msanii mwingine ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuzoa tuzo zaidi ya moja ni Christian Bella, ambaye ngoma yake ya “Nani Kama Mama” ilitingisha kila kona ya nchi na imo kwenye tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka, ambayo pia inawaniwa na Ali Kiba (“Mwana”), Weusi (“Gere”), Fid Q (“Bongo Hip Hop”) na Jux (“Nitasubiri”).
Wakati wa uteuzi wa wateule wa kuwania tuzo hiyo, watu walikuwa na maswali kuhusu kuachwa kwa nyimbo nyingi ambazo zilitamba mwaka jana.
Kipengere chenye utata zaidi ni kile cha Bendi Bora ya Muziki wa Dansi ya Mwaka ambayo inawaniwa na FM Academia, The African Stars, Mapacha Watatu, Mashujaa Band na Msondo Ngoma. Mchuano huu ni mkali kutokana na bendi hizi zote kufanya kazi kubwa mwaka 2014.
Tuzo hii inasindikizwa na ile ya Mwimbaji Bora wa Kiume Bendi inayowaniwa na Jose Mara, Kalala Junior, Khalid Chokoraa, Chaz Baba na Nyoshi El Sadat.
Katika nyimbo ambazo zimechukua umaarufu mkubwa mwaka 2014 zimeingia kama nyimbo bora za Afro Pop ambazo ni “Mwana” – Ali Kiba, “Mdogo Mdogo” – Diamond, “Niseme” – Yamoto Band, “Nitakupwelepweta” – Yamoto Band, “Kanyaboya” – Mesen Selekta na “Hawajui” wa Vanessa Mdee.

No comments:

Post a Comment