.

.

.

.

Saturday, September 20, 2008

NGOMA NZITO "BOT"


Siku moja tu baada ya kuburuzwa kortini kwa watumishi wanane wa Benki Kuu ya Tanzania, BoT, kutokana na tuhuma za kughushi vyeti ili waajiriwe na taasisi hiyo, imedaiwa kuwa zoezi hilo litaendelezwa katika taasisi nyingine nyeti ambako inadaiwa watoto na ndugu wa vibosile wameajiriwa kiujanja-ujanja bila kuwa na sifa. Habari zilizolifikia Blogu hii zinadai kuwa, vigogo kadhaa wako hatarini kuumbuliwa kutokana na ukweli kuwa, katika Benki Kuu peke yake, wako watumishi zaidi ya 12 ambao inadaiwa wamechomekwa kiujanja ujanja. Imedaiwa kuwa watumishi hao ama ni watoto au jamaa wa vigogo. Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya watumishi ndani ya BOT wanadai kuwa licha ya wenzao wanane kufikishwa kortini kwa tuhuma hizo, bado kuna wengine zaidi ya 12 ambao wanadaiwa kuwa nao wamechomekwa kiujanja kwa kutumia ama nafasi za wazazi au ndugu zao Serikalini au umaarufu waliokuwa nao kisiasa. ``Kwa ufahamu wangu ndani ya BOT, wapo watuhumiwa wengine kadhaa ambao nao wanapaswa kufuatiliwa zaidi ili kujua kama utumishi wao unatokana na sifa zilizopo... maneno hayaishi kusemwa kuwa wengine wamechomekwa kiujanja na wazazi wao kwa namna ileile ya kubebana,`` kimedai chanzo chetu kimoja. Wakati vyanzo vyetu vikidai hayo, baadhi ya wanasiasa wamesema licha ya hatua hiyo nzuri ya BOT, bado kuna haja ya kufanyika kazi zaidi ya kujisafisha ili hatimaye, mahakama ifanye kazi yake na kubaini ukweli wa yale yanayodaiwa na watu mbalimbali kuwa taasisi hiyo ina baadhi ya watumishi waliowekwa na wakubwa Serikalini na si kwa sababu ya sifa zao. Wamesema, kinyume cha kufanyika kwa mchakato huo, ni wazi kwamba vijineno havitaisha na matokeo yake, taasisi hiyo nyeti itaendelea kulaumiwa kwa madai ya kuwa kichaka cha ajira za watu wasio na sifa. Professa Mwesiga Baregu ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema BoT inapaswa kuendelea na mchakato huo wa kuwaondoa watumishi wanaodaiwa kutokuwa na sifa. Akasema kwa anavyofahamu, ni kwamba awali kulikuwa kuna taarifa ya watoto zaidi ya 14 wa vigogo wanaofanya kazi katika benki hiyo wakiwa hawana sifa. Akasema suala la kughushi vyeti si zuri kwa mustakabali wa taifa, hivyo BoT inatakiwa kufanyia kazi zaidi tuhuma hizo ili kama kweli wapo watoto wa vigogo wasio na sifa, iwabaini na kuwachukua hatua stahili. Aidha, Prof. Baregu amesema ni vyema zoezi hilo lisiishie BoT pekee na badala yake, liendelee katika mashirika mengine ya umma na taasisi za kiserikali ambazo nazo zinadaiwa kuwa na watumishi kadhaa wanaofanya kazi kiujanja-ujanja kwa sababu ya kukosa sifa.

No comments:

Post a Comment