HABARI zilizofika jijini London Usiku huu zinasema kwamba wachimbaji wadogo wanane wa Mgodi wa Dhahabu Buhemba katika Kijiji cha Magunga wilayani Musoma mkoani Mara, wamekufa baada ya kukosa hewa safi kutokana na shimo kujaa moshi.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow alisema kwa njia ya simu kutokaMusoma kuwa tukio hilo la kusikitisha limetokea saa 12 na nusu asubuhi leo katika machimbo hayo baada ya mtu asiyejulikana kuchoma miti inayotumika kuzuia kifusi kisianguke shimoni.Kamanda huyo wa Polisi aliwataja waliokufa kuwa ni Francis Michael wa Bunda, Juma Mnubiwa Ukerewe, Mabura Gayo wa Bunda, Nokwe Ryoba wa Nkongole, Tarime na Masunga Ngwake wa Kijereshi mkoani Mwanza.Alisema wachimbaji wawili majina yao hayajapatikana kutokana na juhudi za kuopoa miili yao kushindwa kutokana na kukosekana vifaa vya kuokolea na kwamba shimo hilo lina urefu wa zaidi ya futi 200 kwenda chini.Kamanda Barlow alieleza kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi limekwenda kutafuta vifaa vyakuokolea maiti hizo katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ambako inaaminika kuwa vipo.Aidha, Kamanda huyo alisema serikali imesitisha uchimbaji dhahabu kutokana na vifo hivyo kwa muda usiojulikana hadi itakavyoamriwa vinginevyo.Hii ni mara ya pili kwa machimbo hayo kuua vijana wanaojihusisha na uchimbaji huo mdogo ambapo mwanzoni mwa mwaka jana zaidi ya watu wanne walikufa kwa kufukiwa na kifusi wakiwa shimoni.
No comments:
Post a Comment