.

.

.

.

Tuesday, October 21, 2008

TUZIKUMBUKE SIKU ZA MWISHO ZA BABA WA TAIFA


Agosti 26 na 27, 1999
Vyombo vya habari vya Tanzania, kwa mara ya kwanza, vinaripoti wazi kwa umma kuwa hali ya Mwalimu sio nzuri, lakini wasaidizi wake wanaota kigugumizi kuthibitisha hilo; wakidai kwamba wao sio madaktari.
Septemba mosi, 1999
Mwalimu Julius K. NyerereMwalimu, akisindikizwa na mkewe, Mama Maria na daktari wake, David Mwakyusa, wanaondoka nchini kwenda Uingereza, kuchekiwa afya yake, na familia ya Mwalimu inawaambia waandishi wa habari kuwa angerudi nyumbani Septemba 28, 1999.
Septemba 22, 1999
Rais Benjamin William Mkapa, akizungumza na CNN, anaitangazia rasmi dunia kuwa hali ya Mwalimu kule Uingereza "sio nzuri".Septemba 24, 1999 Mwalimu anazidiwa akiwa huko Uingereza, na anakimbizwa katika hospitali ya Mtakatifu Thomas ambako analazwa akiwa "hoi".
Septemba 25, 1999
Rais Mkapa anamtembelea Mwalimu huko hospitalini London na anampa salamu za pole kutoka kwa Rais mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter. Siku hiyo hiyo usiku, kwa sauti yenye kutetemeka na majonzi, Rais Mkapa anaitangazia rasmi dunia kuwa Mwalimu anaumwa kansa ya damu.
Septemba 26, 1999
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini anapitia London na kufika Hospitali ya Mtakatifu Thomas kumpa Mwalimu pole na kumjulia hali.
Septemba 27, 1999
Gazeti la Alasiri, kwa kutumia vyanzo vyake, linaandika kuwa hali ya Mwalimu ni mbaya mno. Aidha Mwalimu anawekwa chini ya mitambo ya kusaidiwa kupumua.
Septemba 28, 1999
Mke wa Mwalimu, Mama Maria, na wanawe Anna na Rose, wanaamua kukaa hospitalini na kumuangalia Mwalimu kwa saa 24. Siku hiyo hiyo Ikulu ya Dar es Salaam inatoa habari za kupotosha kuwa hali yake inaendelea kuwa nzuri kidogo; huku ikimtuma Waziri wa Tawala za Mikoa, Kingunge Ngombale Mwiru kwenda London kusimamia utoaji wa habari za ugonjwa na hali ya Mwalimu kwa ujumla.Siku hiyo hiyo, Mzee Rashid Kawawa analitaka taifa kumuombea Mwalimu apone haraka huku akionyesha kusikitishwa sana na hali ya afya ya Mwalimu kuzorota kwa kasi."...Tunamhitaji zaidi Mwalimu sasa kuliko wakati wowote mwingine uliopita", anasema Kawawa.Wakati huo huo Ikulu nayo inatangaza kuwa Mwalimu amepatwa na ugonjwa mwingine ambao ni sawa na ugonjwa wa homa ya manjano, lakini madaktari wake huko London wanasema “hali yake ni ya kawaida”.
Septemba 30, 1999
Ikulu Dar es Salaam inatoa taarifa kwamba hali ya Mwalimu imeanza kuwa ya nafuu, na kwamba sasa anaweza kugeuka mwenyewe kitandani kwa mara ya kwanza tangu alazwe. Aidha, ameanza kula kidogo kwa kutumia mpira maalumu.
Oktoba mosi, 1999
Ikulu Dar es Salaam inatoa kauli mbili tofauti kuhusu hali ya Mwalimu. Ya kwanza inasema hali ya Mwalimu inabadilika kila wakati, na kwamba amekosa tena kauli na kuhamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi.Ya pili inawanukuu madaktari wakisema kuwa wanapigana vikali kuyanusuru maisha ya Baba wa Taifa.Siku hiyo hiyo Rais Mkapa anawataka wananchi kuendelea kumuombea duwa Baba wa Taifa.
Oktoba 11, 1999
Gazeti la Rai linaripoti kwamba kauli nyingi za Mwalimu kwa wanavijiji, kabla ya kuondoka Butiama, zilikuwa zinaashiria kwamba asingerudi.
Jack Nyamwanga, ambaye amekuwa mtu wa karibu sana na Mwalimu kijijini Butiama, kwa muda mrefu, analiambia Rai kwamba katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwalimu aliacha maagizo mengi yasiyokuwa na uwezekano wa kutekelezeka.Aliacha maagizo ya kupanua mashamba kwa kiwango ambacho kilikuwa ni nje ya uwezo wa kijiji hicho.
“Alituambia mambo mengi sana. Sasa ndio ninagundua kuwa inawezekana alijua kuwa hatarudi akiwa mzima".
Oktoba 14, 1999
Rais Mkapa anawatangazia rasmi Watanzania habari za kusikitisha za kifo cha Mwalimu. “Mwalimu katutoka. Hayupo tena. Amerudi kwa Muumba wake”.
Sambamba na hilo, Rais Mkapa anatangaza pia kwamba ametuma ujumbe mzito wa watgu kumi kwenda London, ukiongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma ili kuurudisha nyumbani mwili wa Mwalimu.
Mbali ya Dk. Omar, wengine walioko kwenye ujumbe huo ulioondoka Oktoba 16 ni mkewe, Mama Salma, Waziri wa Ujenzi, Bi. Anna Abdallah, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, John Cheyo, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Fatuma Maghimbi, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (CCM), Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Mapuri, Mbunge wa Musoma Vijijini, Balozi Paul Ndhobo. Wengine ni Abbasi Mhunzi, Haji Mkema, Hamad Fadau ambao ni wabunge wa CUF.
Oktoba 17, 1999
Rais Mkapa anaongoza maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam kuupokea mwili wa Mwalimu Nyerere unapowasili saa 5 asubuhi kutoka London. Maelfu wanausindikiza mwili wa Mwalimu kwa maandamano hadi nyumbani kwake Msasani kupitia barabara kadhaa za Dar es Salaam zikiwemo Nyerere, Nelson Mandela, Kawawa nk.
Oktoba 18, 1999
Mwili huo unaondolewa Msasani, leo, Jumanne, saa 2 asubuhi, na kusindikizwa na Rais Mkapa, kupelekwa Kanisa la St. Joseph kupitia barabara za TPDC, Ali Hassan Mwinyi, Luthuli, Kivukoni Front, Sokoine Drive hadi Kanisa la St. Joseph. Misa hiyo inamalizika saa 4.30 asubuhi na mwili unapelekwa Uwanja wa Taifa kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho.
Oktoba 20, 1999
Majonzi, simanzi na huzuni vinatawala yuso za viongozi wa mataifa mbalimbali kwenye Uwanja wa Taifa kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kabla haujapelekwa Butiama kwa mazishi. Baadhi yao ni Daniel arap Moi, Jerry Rawlings, Joachim Chissano, Bakili Muluzi na Sam Nujoma.Oktoba 22, 1999
Mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere unawasili Butiama na kupokelewa kwa taratibu za kijadi huku kukiwa na mvua kubwa na ngurumo kali za radi. Mwili huo uliwasili majira ya saa 1.45 usiku, ukitokea Musoma ambako ulipokelewa kwa taratibu za kijeshi. Unapowasili Butiama unapokelewa na Chifu wa Zanaki, Japhet Wanzangi.
Oktoba 23, 1999
Mazishi ya Mwalimu Nyerere yanafanyika kijijini Butiama na kuhudhuriwa na baadhi ya marais wa nchi za jirani akiwemo Yoweri Museveni wa Uganda. Kabla ya mwili kuwekwa ndani ya kaburi la zege, kikosi maalumu cha jeshi chafanya gwaride maalumu la heshima na kufuatiwa na wimbo wa taifa na ibada ya mazishi.Siku moja kabla ya mazishi, matetemeko mawili mfululizo yanatokea Butiama. Chifu wa Wazanaki, Japhet Wanzangi anasema matetemeko hayo yanahusiana moja kwa moja na kifo cha Mwalimu, na kwamba ni inshara ya kifo cha kiongozi anayeheshimiwa sana katika ukoo na kabila la Kizanaki.
SOURCE:Raia mwema

No comments:

Post a Comment