BASI la Kampuni ya Zuberi lililokuwa kikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza limeanguka leo saa moja asubuhi na kuua, Watu zaidi ya 25 wamekufa. Ajali hiyo imetokea kwenye Mlima Sekenke jirani na mji mdogo wa Shelui baada ya basi hilo kugonga ukuta wa barabara na kutumbukia kwenye korongo urefu wa mita 200. Mmoja wa mashuhuda aliyekuwa eneo la tukio la Hussein Magembe ameliambia Dar Leo kwa simu wakati likienda mitamboni kuwa jitihada za kuokoa majeruhi na kutoa maiti ndani ya basi hilo zilikuwa zikiendelea. Magembe amesema basi hilo liliharibika vibaya na lililazimika kukatwa kwa gesi kunasua miili ya watu walionasa ndani. Shuhuda huyo amesema ilikuwa vigumu kubaini mara moja namba ya basi hilo Scania kutokana na kuharibika vibaya lakini aliweza kusoma herufi tatu za mwisho kwenye namba hiyo ambazo ni ALD Amesema majeruhi wamepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Iramba mjini Kiomboi na wengine walikuwa wakipewa matibabu Zahanati ya Shelui. " Hii ni ajali mbaya saana, basi halitamaniki kabisa limeharibika vibaya, maiti wamenasa ndani, wametolewa kama kumi tu wengine tunalazimika kukata mabati kwa kutumia gesi ili kuwatoa," amesema Magembe. Ameongeza kuwa " Kama una roho nyepesi huwezi kuangalia basi hili , inatisha na inaelekea majeruhi ni kidogo kuliko waliokufa . Amesema ajali hiyo ni ya kwanza kubwa kutokea tangu barabara hiyo ilipochongwa upya. Akzungumzia chanzo cha ajali hiyo amesema kwa mujibu wa walionusurika, dereva alikuwa akijaribu kubadili gea na kwa bahati mbaya ziligoma na kulazimika kubamiza basi hilo kwenye ukuta wa barabara ndipo lilipaa na kupanda upande wa pili wa barabara kabla ya kutumbukia kwenye korongo hilo. Alitaja baadhi ya watu walionusurika kwenye ajali hiyo kuwa ni pamoja na utingo aliyemtaja kwa jina moja la Salumu na Imamu mmoja wa mjini Nzega na walikuwa wakipatiwa matibabu zahanati ya Shelui. Mkuu wa Mkoa wa Singida Parseko Kone alilazimika kukatiza ziara yake wilayani Iramba na kuelekea eneo la tukio akiambatana na Mkurugenzi wa wilaya hiyo Fortunatus Fwema. Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Celina Kaluba kuzungumzia ajali hiyo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kuwa imezimwa. Dar Leo lilijaribu kuwasiliana kwa simu na Askari wa Kikosi cha Usalama barabarani Kituo cha Shelui nao pia hawakupatikana kutokana na simu zao kufungwa. Hata hivyo baadhi ya waandishi wa habari mjini Singida walithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa walikuwa wakijiandaa kwenda eneo la tukio. Dar Leo lilipozungumza kwa simu na mmoja wa wahudumu wa mabasi ya Zuberi aliyeko Dar es Salaam, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo hata hivyo alisema bado hawana uhakika ni watu wangapi wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo.
KWA HISANI YA DARLEO
No comments:
Post a Comment