HATIMA ya uchunguzi kwenye akaunti iliyoibua utata ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge iliyokutwa na zaidi ya sh. bilioni moja visiwani Jersey bado limeendelea kuwaumiza vichwa makachero na sasa hatima ya lini ukweli utajulikana, imebaki kitendawili. Wiki mbili zilizopita ililipotiwa kuwa Serikali ya Jersey kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, imeahidi kuwa ingefuatilia hatua zilizokuwa zimefikiwa ili kubainisha uchunguzi ulipofikia. Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jersey, Bi Carthy Cair alisema kwa sasa tamko kuhusu kilichobainika haliwezi kuwekwa hadharani tena. "Nimewasiliana na wataalamu wa sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuhusu wapi wamefikia, inaonekana kwa sasa bado hawawezi kutoa taarifa," alisema Bi. Carthy. Hatua ya viongozi wa visiwa hivyo kubadili msimamo tofauti na awali waliposema wangekuwa tayari kuweka hadharani inaonesha jinsi uchunguzi huo ulivyogubikwa na utata na usiri mkubwa. Si Jersey tu hata nchini Uingereza nako sakata la rada kwa ujumla linaonekana kuwatoa jasho hata makachero wa Idara ya Kupambana na Ufisadi (SFO) ambao nao kwa sasa wamekwishachukua zaidi ya miaka miwili wakilichunguza suala hilo. Chenge aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu, amekuwa akichunguzwa iwapo naye ni mmoja wa maofisa wa Tanzania waliofaidika na kamisheni ya zaidi ya sh. bilioni 12 ambayo ilitolewa katika kuwashawishi vigogo wa hapa nchini wakubali ununuzi wa rada ambayo imebainika kuwa kuukuu na iliyopandishwa bei. Wachunguzi hao walipompekua Bw. Chenge Dar es Salaam na katika akaunti zake za nje ndipo walipobaini kuwepo kwa kiasi cha pauni takribani 500,000 (zaidi ya sh. bilioni moja) alizokuwa amezihifadhi kwenye visiwa hivyo ambazo walizitilia shaka na kuanza kuchunguza uhalali wake. Alipobanwa na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu fedha hizo, Bw. Chenge alionesha kuzidharau kuwa ni kiasi kidogo mno ambacho asingepaswa kufuatwafuatwa akiziita 'vijisenti,' neno lililoibua mjadala mkali na shinikizo zilizomfanya ajiuzulu wadhifa wake.
No comments:
Post a Comment