ALBINO aliyekatwa mikono na kunusurika kuuawa na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Murugwanza wilayani Ngara, Mariamu Stanford (28), ameishauri serikali imhakikishie ulinzi, hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Mlemavu huyo wa ngozi, amelazwa katika hospitali hiyo baada ya watu wasiojulikana, kumkata mikono yake yote miwili.
Hata hivyo habari zilisema kitendo hicho, kimefanywa na watu waliotawaliwa na imani za ushirikina kuwa viungo vya albino, vinasaidia katika jitihada za kutafuta utajiri, imani ambayo ni potofu na kipuuzi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki iliyopita, Mariamu, alisema pamoja na jitihada za serikali na uongozi wa hospitali hiyo za kunusuru maisha yake, bado anahofia usalama wa maisha yake hasa baada ya kuruhusiwa.
“Nahofia wataniua wakiniona kijijini, najua watanikata kichwa kwa sababu niliwaona watu walionifanyia kitendo hiki na nikawatajia polisi, kwa hiyo naogopa kutoka hapa.
Hata hivyo naamini serikali itanisaidia watajua wanipeleke wapi,” alisema Stanford akiwa ameketi kitandani katika wodi ya majeruhi, huku akiwa amembeba mtoto wake mgongoni.
Mlemavu huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ntobele, alisema usalama wa maisha yake ya baadaye, unategemea mno busara ya serikali, hasa kuhusu mahali anapoweza kuishi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Alisema licha ya kuhofia kuuawa, lakini pia kitendo cha kumkata mikono yake, kimemweka katika mazingira magumu ya kuishi, kwa sababu sasa hatakuwa tena na uwezo wa kufanyakazi za kujipatia riziki.
Aliiomba serikali, watu binafsi na asasi mbalimbali, kuangalia uwezekano wa namna ya kumsaidia, ili kumwezesha kuishi kama binadamu wengine na kufanya kile anachokipenda.
“Kabla ya kukatwa mikono nilikuwa namsaidia mama yangu kufanya kazi za kulima shambani baada ya kuacha shule, kulikosababishwa na matatizo ya macho, baadaye nilikuwa nikienda kanisani kuimba kwaya na wenzangu, lakini hayo sasa hayatawezekana kwa sababu sina tena mikono,” alisema Stanford.
Majeruhi huyo ambaye alikuwa na mimba iliyoporomoka kutokana na msongo wa mawazo uliotokana na kitendo cha kukatwa mikono, alielezea matumaini yake kuwa, Watanzania watamwezesha kuwekewa mikono bandia na kumsaidia katika mambo mengine ikiwa ni pamoja na kumtunza mtoto wake.
“Sasa niko hivi nani atanioa, nitamtunzaje mwanangu, naiomba serikali na watu wenye mapenzi mema wanisaidie,” alinena.
Mganga wa zamu katika hospitali hiyo, William Munyongera, alisema jeraha la mkono wa kulia wa Stanford,limepona kabisa na lile la mkono wa kushoto halijapona na kwamba hiyo imetokana na maambukizi ya vidudu vilivyokuwemo katika panga lililotumika kukata viungo vyake.
Alisema hata hivyo kuna matarajio makubwa kuwa ataruhusiwa kuondoka hospitalini katika kipindi kifupi kijacho.
“Tunatarajia kumruhusu ili aende nyumbani kwa sababu majeraha yake yamepona kwa asilimia 85, mkono wake wa kushoto haujapona kabisa na hi ni kwa sababu ya kuambukizwa vijidudu vilivyotokana na panga lililotumika kumkatia,” alisema
No comments:
Post a Comment