Naomba niandikie kutoka kwenye hisia kidogo; Naomba niandike toka kwenye vionjo vyangu vilivyojeruhiwa; Naomba niandikie kutoka kwenye moyo uliojawa na hasira, kero na ambao unajihisi kinyaa!; Naomba niandike kama mtu ambaye akili zake hazijakaa sawasawa na ambaye anaweza kuitwa "fyatu"! Naomba niandike kuhusu haya ya Shirika letu la ndege la ATCL ambalo limekuwa kituko cha taifa na aibu ya nchi yetu! Watawala wetu mmerogwa? Tumefikaje hapa, je hili limefika kama kwa ghafla na kwamba hakukuwa na dalili zozote? Kwamba leo bila haya mnaitisha vikao vya dharura na kutoa "siku saba" za kupata maelezo toka kwa wazembe na waliofuja mali za shirika hili kana kwamba hamkuliona hili? Ati leo mnathubutu kuelezea kilichofanyika ATCL kuwa ni uzembe wakati kwa mwaka mzima vumbi lake mlishaliona toka mbali? Mmerogwa nyinyi? Nauliza kama mmerogwa kwa sababu hakuna maelezo yoyote ya kiakili ambayo yana ushawishi wa kimantiki na yenye uzito wa ushahidi wa kisayansi yanaweza kuelezea ubutu wa matendo yenu na ukimya wa maneno yenu kwa mwaka mzima tangu king'ora cha tahadhari tulipokipuliza mwezi Disemba mwaka jana! Ni watu waliopumbazwa na dawa za mitishamba au waliorogwa 'kisayansi' ndio pekee wanaweza kufafanua ni kitu gani kiliwakumba. Mmepitiwa na jini gani lililowafanya mduwae na kuangusha midomo yenu ya chini na denda zikidondoka kama wale wasemwao "washangaao feri"? Tuliimba na kupaza sauti, makoo yetu yakakauka. Tukawaambia tena bila kuuma uma maneno kuwa ATCL kuna uozo; tena uozo mkubwa wa kiuongozi. Tukaweza mipango yao ya kukodisha dege lenye matatizo ya kiufundi zaidi ya 100 tena kwa bei mbaya; tukawawekea na mikataba yao waliyoingia kuhusu dege hilo hilo, lakini muda wote huo nyinyi mkaendelea kukaa kimya na kuacha ATCL ijiendeshe kama kikaragosi kinachoenda kwa kupiga ufunguo! Tukawawekea na ushahidi jinsi gani watendaji wa ATCL wamefuja mali zetu huku wakikinga mikono yao kuyupa zaidi; tukawaonesha jinsi mikakati yao ilivyokuwa mibaya na mibovu; tukawaonesha ni jinsi gani David Mattaka na genge lake la makuwadi wa ufisadi wameshindwa kuliongoza shirika hilo. Kwa mwaka mzima tumefanya hivyo pasipo mafanikio
SOURCE: MWANAKIJIJI
No comments:
Post a Comment