.

.

Sunday, March 22, 2009
AFARIKI AKITOKA KUCHUKUA MAHARI
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Romano Michese (70), mkazi wa kitongoji cha Makazi Mapya mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, amekufa maji wakati anatoka kuchukua mahari ya binti yake, aliyemuoza katika kijiji cha jirani. Tukio hilo lilitokea machi 19, mwaka huu saa 12 jioni, ambapo Michese alitumbukia katika mto Kisa na kusombwa na maji kwa umbali wa kilometa mbili ambako aliokotwa akiwa amekufa. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Isunto Mantage, alisema kuwa marehemu alikuwa anatoka katika Kijiji cha Mtimbwa kuchukua mahari baada ya kumuoza binti yake, ambapo kabla ya kuanza safari inadaiwa alikunywa pombe akiwa katika kijiji hicho. Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa amekwenda kuchukua mahari hiyo akiwa peke yake na wakati anarudi alipofika katika mto huo, alishindwa kuvuka kutokana na kuto kuwa na daraja, alipokuwa katika jitihada za kuvuka kwa kutumia miti inayotumika kuvuka mto huo, aliteleza na kudumbukia mtoni. Kwa mujibu wa madai hayo, kesho yake asubuhi ndugu wa mzee huyo walianza kuingiwa na hofu kutokana na Michese kutorejea na kuwasilisha mahari hiyo, ambayo ilikuwa inasubiriwa ili ndugu wagawane na ndipo walipotuma mtu aende ukweni akaulizie iwapo alifika kuchukua mahari hiyo. Walipothibitishiwa kuwa aliondoka huko akiwa na fedha hiyo ya mahari, ndipo walipoanza kumtafuta na walipofika katika mto Kisa na kuanza kumtafuta, walifanikiwa kuupata mwili wake ukiwa umetuama katika vichaka vya mto huo. Baada ya kumkagua mfukoni, walikuta kukiwa na kitita cha fedha mfukoni mwake ambacho ndicho alichokabidhiwa kwa ajili ya mahari ya binti yake huyo alioolewa katika Kijiji cha Mtimbwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment