.

.

.

.

Saturday, April 25, 2009

MH.PHARES KABUYE AFARIKI KATIKA AJALI YA BASI


MBUNGE wa Jimbo la Biharamulo Magharibi mkoani Kagera Bw. Phares Kabuye amefariki kwa ajali ya basi akiwa safarini kutoka Kagera kwenda Dar es Salaam kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Tanzania Labour Party (TLP) uliopangwa kufanyika kesho.Katika Mkutano huo, Bw. Kabuye alikuwa ameomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwenye uchaguzi huo, uliosubiriwa kwa shauku na wanachama wengi wa chama hicho.

Marehemu Kabuye, Mbunge aliyesimamishwa wa TLP, alifariki jana saa mbili asubuhi eneo la Magubike, wilayani Kilosa, Morogoro. Katika ajali hiyo, watu wengine wawili walikufa na wengine 54, kujeruhiwa.Ajali hiyo ilihusisha basi la RS Investment, lenye namba za usajili T934 ABK lililoserereka na kupinduka likiwa kwenye mwendo.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Samuel Sitta amethibitisha tukio hilo na kueleza kusikitishwa kwake na kifo cha Mbunge huyo ambaye hadi mauti yakimfika , alikuwa akipigania rufani yake mahakamani kupinga kuvuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Kagera .

Abiria walionusurika, walisema basi hilo liliserereka na kupinduka baada ya mtu aliyekuwa akiendesha anayedaiwa kuwa utingo, kushindwa kulimudu.Walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa basi hilo lilikuwa katika mwendo na waliokaa sehemu ya mbele, walisikia dereva aliyekaa pembeni akimwelekeza utingo huyo kushika breki haraka.Kufumba na kufumbua, basi hilo lilihamia upande wa pili wa barabara na kupinduka tairi zikiwa juu na kugeuka lilikotoka. Dereva na utingo huyo walikimbia baada ya ajali hiyo na hawajulikani waliko.

1 comment:

  1. R.I.P mzee mungu amekuweka mahala ambapo katuahidi wote

    ReplyDelete