.

.

.

.

Wednesday, June 10, 2009

AJALI YAUA SITA DODOMA

WATU sita wamefariki dunia na wengine 37 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka katika kijiji cha Mtumba kilichopo kilometa 20 kutoka Dodoma mjini. Abiria hao walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Singida wakiwa kwenye basi la kampuni ya Hajj's lenye namba za usajili T 441 AYN aina ya Scania. Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfrey Mtei, ajali hiyo ilitokea saa 5.45 asubuhi, baada ya kupasuka gurudumu na kupoteza mwelekeo kabla ya kupinduka mara tatu. Dk. Mtei alisema alipata taarifa za ajali hiyo saa 6.30 mchana, ambapo alituma magari eneo hilo na kuanza kupokea majeruhi pamoja na maiti. Alisema abiria watano walikufa papo hapo na mwingine mmoja baada ya kufikishwa hospitali hapo. Dk. Mtei alisema majeruhi 18 akiwemo mwanamke mmoja ambaye hali yake ni mbaya wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la upande wa dereva na kusababisha gari kupinduka mara tatu. Dk. Mtei alisema kabla ya basi hilo kupinduka liliyumba na kumgonga mwendesha baiskeli aliyekufa papo hapo. Dk. Mtei aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Amida Ramadhani, Agnes Bless, Bertha Lucas, Mwanaidi Kisoja, Amina Hussein, Rehema Hassan, Costancia Ngole, Lidya Athuman, Juliana Rona ambao wamelazwa wodi namba 10. Wengine Rosian Bless na Ruthiwart Abdul ambao wamelazwa wodi namba 8. Wengine ni Hassan Kambi, Jacob Daniel, Ezekiel Daniel, Khali Mbegu na Idd Mussa ambao wamelazwa wodi namba 1. Majeruhi wengine ni Charles Kisuda na Mwanahamis Seleman ambao wamelazwa wodi namba 2. Hata hivyo Dk. Mtei alisema waliokufa hawajatambuliwa. Kutoka Morogoro Mwandishi Wetu, Farida Msengwa anaripoti kuwa watu watatu wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa, baada ya lori walilokuwa wakisafiria kugonga lingine kwa nyuma katika eneo la Kwambe Njianne wilayani Kilosa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alisema tukio hilo lilitokea Juni nane,mwaka huu, saa 8:45 usiku. Akielezea tukio hilo, alisema lori hilo lenye namba za usajili T 668 AUS aina ya Mitsubish Fusso, likiendeshwa na Bahati Adam mwenye umri kati ya miaka 30-35 akitokea Mpwapwa kuelekea Dar es Salaam liligonga loori lingine kwa nyuma. Kamanda Andengenye alisema lori lililogonga ni namba T 199 AHX lenye trela namba T 231 AHC, lililokuwa likiendeshwa na John Joseph(45) mkazi wa Magomeni Dar es Salaam likitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam. Aliwataja waliokufa kuwa ni dereva wa lori namba T 668 AUS Bahati Adam, mkazi wa Mpwapwa mkoani Dodoma, Amani Mwongo (29) mkazi wa Ng'ambi wilayani Mpwapwa, ambaye ni mfanyabiashara na mwanaume mmoja. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya utambuzi. Aliwataja majeruhi kuwa ni Rose Julius (12), mkazi wa Kongwa na mwanafunzi wa shule ya msingi Kongwa, Ally Balali (35), mkazi wa Mpwapwa na Nyakatare Ranje (35), kutoka Kongwa, ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Morogoro. Kamanda Andengenye alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva Adam ambaye kwa sasa ni marehemu.

No comments:

Post a Comment