KESI za mauaji ya albino zimeanza kusikilizwa jana mbele ya Jaji Gadi Mjemas Mkoani Shinyanga katika mahakama kuu ya Tanzania ambapo watuhumiwa wanne walisomewa mashtaka. Washtakiwa hao ni Mboje Mawe,Chenyenye Maganyale, Sayi Gamanya na Sayi Mofizi ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya kumuua mlemavu wa ngozi ajulikanaye kwa jina la Lyaku Willy Akisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo, mbele ya Jaji Mjemas, wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki alidai kuwa, watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Novemba Mosi na Desemba 5 mwaka jana katika kijiji cha Nkwindaguye Wilaya ya Bariadi Mkoani Shinyanga. Wakili Kakolaki alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo baada ya Sayi Gamanya aliyekuwa akiishi na marehemu nyumba moja ambaye ni shemeji wa marehemu kumwambia angempeleka hospitali ya Somanda kwa ajili ya matibabu ya kidonda cha marehemu kilichokuwa kinamsumbua kwa muda mrefu. Wakili Kakolaki aliendelea kusoma hati hiyo kuwa siku ya tukio washitakiwa Mboje Mawe, Chenyenje Maganyale na Sayi Mofizi walilala nyumbani kwa Gamanya kwa lengo la kumsindikiza marehemu kwani hospitali ilikuwa mbali hivyo wangeanza safari saa saba usiku ili wafike asubuhi. Wakiwa njiani eneo la mto Kidamlida inadaiwa mshtakiwa Sayi Gamanya alimwambia marehemu aoshe kidonda chake ili aweze kutibiwa vizuri afikapo hospitali, ndipo marehemu alipoinama mtoni ili aweze kuosha kidonda chake. Inadaiwa kuwa mara marehemu alipoinama mtoni mshtakiwa Chenyenye Maganyale alimzamisha ndani ya maji hadi marehemu alipopoteza fahamu na ndipo walimtoa na kumchinja shingo pamoja na miguu kwa jambia na panga na kukiweka kiwiliwili kilichobaki ndani ya mfuko wa sandarusi kisha kukitupa kwenye kisima cha kunyweshea mifugo. Aidha baada ya watuhumiwa hao kumaliza zoezi hilo walihifadhi viungo hivyo ndani ya mfuko wa Rambo na kwenda kuvifukia maeneo tofauti tofauti karibu na nyumba ya Mboje Mawe na vifaa vilivyotumika vilifichwa katika nyumba ya mtuhumiwa huyo. Wakili Kakolaki aliendelea kusoma maelezo kuwa Novemba 29, mwaka jana, taarifa za kuonekana kwa mwili huo katika mto Kidamlida zilienea kijijini hapo na kutolewa kwa uongozi wa polisi ambapo polisi wa Wilaya ya Bariadi walifanikiwa kuutoa mwili huo Desemba 5, mwaka huohuo. Wakili Kakolaki alisema baada ya mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi na Daktari wa Hospitali ya Bariadi Anania Maduhu, ilibainika kuwa, sababu ya kifo ni kuvuja damu kwa wingi kulikotokana na kukata sehemu za viungo hivyo. Baada ya taarifa kutoka kwa Daktari Maduhu, mshtakiwa wa tatu ambaye ni Sayi Gamanya alikamatwa ambapo katika mahojiano alikubali kuhusika na mauaji hayo na kudai kuwa viungo hivyo vilitakiwa kuuzwa kwa mganga eneo la Lamadi Mkoani Mwanza na aliwataja washtakiwa Mboje Mawe,Chenyenye Maganyale na Sayi Mofizi kuhusika na mauaji hayo. Jopo la Mawakili wa Serikali lilijumuisha mawakili wandamizi watatu ambao ni,Veritas Mlay, Lenatus Mkude na kuongozwa na Bwana Edwin Kakolapi ambapo jopo la mawakili wa upande wa utetezi lilijumuisha mawakili Serapion Kahangwa,Feran Kweka, Method Kabuguzi na John Ngw’igulila. Washtakiwa walikana mashtaka na kesi inaendelea leo na kwamba mashaidi 14 wataitwa mahakamani ili kutoa ushahidi.
No comments:
Post a Comment