MIAKA 10 tangu kifo chake,Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ameongoza kwa ubora miongoni mwa mawaziri wakuu 10 waliowahi kushika wadhifa huo nchini, akifuatiwa kwa karibu na Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa miezi mitatu iliyopita na Kampuni ya Synovate ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Steadman Group Tanzania, Pinda ametofautiana kwa pointi moja tu nyuma ya mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere anaongoza kwa asilimia 29 na Pinda anamfuatia kwa asilimia 28 na kuwaacha wengine kwa tofauti kubwa akiwamo aliyemtagulia Edward Lowassa. Mawaziri wakuu wanaoshika mkia kwa ubora ni John Malecele, Cleopa Msuya na Joseph Warioba ambao kila mmoja amepata asilimia moja.
Hayati Edward Sokoine, ambaye alikufa kwa ajali ya gari mwaka 1984 akiwa ana sifa kemukemu kutokana na kuongoza vita dhidi ya walanguzi na wahujumu uchumi, anashika nafasi ya tatu kwa ubora akiwa na asilimia 26.
Baada ya Sokoine ambaye anashika nafasi ya tatu, mawaziri wakuu wengine wamepata alama za ubora chini ya asilimia 10.
Nafasi ya nne inashikiliwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye kwa asilimia sita wakati Edward Lowassa ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond mwaka jana, anafungana na Mzee Rashid Kawawa na kushika nafasi ya tano kwa kuwa na asilimia nne.
Nafasi ya tano inashikiliwa na Dk Salim Ahmed Salim ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao kwa sasa unajulikana kama Umoja wa Afrika (AU).
Utafiti huo unamuonyesha pia Pinda kama waziri mkuu anayefahamika zaidi kwa watu kuliko wengine. Katika kundi hilo, Pinda anafahamika kwa watu kwa asilimia 81, akifuatiwa na Lowassa kwa asilimia 73.
Wanaofuatia pamoja na kiwango cha asilimia cha kufahamika ni Sumaye (60), Sokoine (45), Nyerere (37), Kawawa (34) Malecela (24), Warioba (20), Msuya (18) na Dk Salim (14).
Meneja Msaidizi wa Synovate, Agreey Orio aliviambia vyombo vya habari hivi karibuni kuwa kwenye utafiti huo Rais Jakaya Kikwete ana ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa tena kwenye nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, 2010.
Kwa upande wa rais wa Zanzibar, utafiti huo ulionyesha kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, anapewa nafasi kubwa ya kushinda.
No comments:
Post a Comment