.

.

.

.

Tuesday, September 22, 2009

MAUAJI MWANZA

Watu watatu wamefariki dunia mkoani hapa katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke kukatwakatwa mapanga na watu wasiofahamika kutokana na imani ya uchawi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow, alisema tukio la kuuawa kwa kikongwe huyo, Sophia Ng’ono (52) ambaye ni mkulima, lilitokea juzi katika kijiji cha Idetemya wilayani Geita.
Alisema mwanamke huyo aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana alipokuwa akila chakula cha usiku.
Alisema kufuatia mauaji hayo, Laurent John (38), anashikiliwa na polisi.
Katika tukio lingine, wananchi wenye hasira wamemuua mfanyabiashara Mhoja Shabani (34) kwa kumpiga na fimbo na mawe hadi kufa baada ya kumtuhumu kwa wizi wa ng’ombe saba.
Kamanda Rwambow alisema mfanyabiashara huyo anatuhumiwa kuiba ng’ombe wa Pascal James (37).
Alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki majira ya mchana katika kijiji cha Nyang’wale wilayani Geita na kwamba hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Wakati huo huo, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Zainab Moris, amekufa baada ya kuteketea kwa moto uliotokana na mshumaa uliowashwa kuanguka na kuunguza chumba alichokuwa amelala.
Rwambow alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki saa 12 jioni katika eneo la Pasiansi, jijini Mwanza ambapo mama wa mtoto huyo Mariam Moris (31) aliiarifu polisi juu ya tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment