.

.

.

.

Friday, September 25, 2009

RAMBIRAMBI PLUS

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kushirikiana na kampuni ya huduma za bima ya Alexander Forbes imezindua bima ya mazishi kwa ajili ya wateja wake ijulikanayo kwa jina la Rambirambi Plus.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bima hiyo uliofanyika katika hotel ya New Africa jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa huduma za rejareja za kibenki za benki hiyo, Johan Vermaas alisema bima hiyo ni bima ya kujitegemea ambayo inalenga kusaidia kufidia wanafamilia wa mfanyakazi wa benki hiyo aliyejiwekea akiba akifariki.
Alisema bima hiyo inamuwezesha mtu kuchukua mafao kwa kiwango alichochagua na kuyataja mafao hayo kuwa ni Shaba ambayo ni kuanzia Sh.500,000, Fedha Sh 700,000, Dhahabu Sh.1 milioni na Almas Sh.2 milioni.
“Ni utamaduni wa Watanzania kuchangia pesa, vyakula na vifaa vingine vya mazishi vinavyojulikana kama rambirambi kwa familia za wafiwa kuwasaidia katika mipango ya mazishi,” alisema Vermaas na kuongeza;
“Sisi NBC kwa mara nyingine tunatoa huduma mpya kwa wateja wetu wa Tanzania ikiwa ni pamoja na hii bima ya mazishi kwa wanafamilia ijulikanayo kama
Rambirambi Plus,” alisisitiza.
Vermaas alisema bima hiyo itawasaidia wanafamilia katika kufanya maandalizi ya kabla na kuweka akiba kwa ajili ya gharama za mazishi na kwamba bima hiyo ina bonas za aina mbalimbali zitolewazo na benki hiyo zinazokimu mahitaji na uwezo wa kifedha kwa wateja wenye vipato mbalimbali.
“ Tunafahamu mahitaji ya wateja wetu, na hii ndio maana tumeamua kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya bima ya Alexander Forbes kutoa bima ya Rambirambi Plus ili kufidia familia ya mwana bima inapotokea amefariki”, alisisitiza Vermaas.
Naye Meneja madai wa bima hiyo, Charles Zanny alisema bima hiyo imemuangalia mtu wa chini kabisa na Mwafrika katika mazingira ya familia pana na kwamba katika familia bima hiyo inawajumuisha pia wazazi wanne na watu wengine kama mjomba na shangazi.
Kwa upande wake Mkurugnzi Mtendaji na Meneja Mkuu wa kampuni ya bima ya Alexander Forbes, alisema masharti ya bima hiyo ni kuwa mteja wa NBC na kwamba hakuna suala la kupima afya isipokuwa mteja atatakiwa kujaza fomu tu.

No comments:

Post a Comment