Mwanafunzi wa Kidato cha tatu katika Sekondari ya Iwindi wilayani Mbeya Vijijini, Aurelia Maftah (20), anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanafunzi mwezeka wa kidato cha kwanza Mwasiti Seifu (16) wa Sekondari ya Maranantha kwa kumchoma kisu tumboni na kutoroka.
Imeelezwa kuwa kabla ya kutenda tukio hilo, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu ambaye alikuwa akipika chakula na kumtaka waende pembeni kwa kuwa alitaka kuzungumza naye na ndipo alipofanya kitendo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea eneo la tukio ambako ni nyumbani kwa marehemu, ndugu wa marehemu, Christopher Hosea, alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu saa 2:00 usiku katika eneo la Iwindi.
Alisema kuwa marehemu na mtuhumiwa ni ndugu ambao walikuwa na ugomvi kwa muda mrefu unaohusishwa na kugombea bwana na kwamba kabla ya tukio hilo kutokea, walikutwa wakipigana katika kisima cha maji na familia ilipewa taarifa na kwenda kuwachukua.
Alisema siku hiyo ya ugomvi, wanafamilia walikaa kikao na kuwataka wasichana hao kueleza sababu za ugomvi na kwamba baadaye walibaini kwamba Aurelia alikuwa na makosa hivyo walimtaka kuomba msamaha, kitendo ambacho alikikaidi na kutoa kisu kutaka kumchoma mwenzake.
Aliongeza kuwa kitendo hicho hakikufanikiwa baada ya mtuhumiwa huyo kunyang’anywa kisu na hivyo kumsihi kutofanya kosa hilo tena na kukubaliana nao kisha kuondoka.
“Cha kushangaza ni kwamba ilipofika majira ya saa mbili usiku, tulisikia kelele za kuomba msaada na tulipotoka kwenda kuangalia nini kimetokea, tulimkuta Mwasiti akitokwa na damu nyingi tumboni” alisema Hosea.
Alisema walimpeleka katika hospitali Teule ya Ifisi iliyoko Mbalizi lakini alifariki dunia wakiwa njiani. Aidha, Hosea alisema kwa mujibu wa maelezo ya marehemu, mtuhumiwa alifika nyumbani hapo akimtaka watoke nje kwa ajili ya mazungumzo ya kumaliza tofauti zao lakini ghafla alichomoa kisu na kumchoma tumboni Mwasiti na kukimbia.
Hosea alipoulizwa na mwandishi kama walitoa taarifa polisi, alisema kuwa walitoa taarifa katika kituo kidogo cha polisi cha Mbalizi na kufunguliwa jalida namba IR/7452/2009 na kuongeza kuwa hivi sasa wapo katika maandalizi ya mazishi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Maranantha, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mlawa, alikiri kuwa mwanafunzi aliyefariki dunia ni wa shule yake na kwamba wakati tukio hilo linatokea, tayari muda wa masomo ulikuwa umekwisha hivyo yeye hawezi kulizungumzia zaidi suala hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa safarini. Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Elige Mhimila, alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kwamba msichana huyo bado anatafutwa na polisi.
No comments:
Post a Comment