WAFANYABIASHARA wawili maarufu hapa nchini wenye asili ya Kiasia, Yusuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel, wanadaiwa kuingia katika mzozo mkubwa wa kibiashara wakati wakigombea kupata zabuni ya mradi wa kuingiza nchini na kusambaza matrekta, wenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 50.
Habari ambazo zimepatikana kwenye vyanzo vya habari vya kuaminika zimeeleza kuwa, Manji na Patel ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kuomba zabuni hiyo, sasa wanawindana huku wakitishana kumalizana kibiashara.
Baadhi ya watu wa karibu na wafanyabiashara hao mabilionea waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika siku za karibuni walieleza kuwa, kumekuwa na jitihada za chini kwa chini zinazofanywa na wapambe wao kuvujisha katika vyombo vya habari mbinu zao wanazotumia kupata zabuni kubwa za serikali.
Mfanyabiashara mmoja maarufu ambaye yuko karibu na wafanyabiashara hao, alilieleza gazeti hili kuwa, mabilionea hao sasa wamekuwa mahasimu baada ya kuzidiana ujanja katika zabuni hiyo ambapo kila mmoja anatishia kutoa siri za kibiashara za mwenzake.
“Sasa wanatishana, kila mmoja anatishia kutoa siri za mwenzake kibiashara. Wote wanapata tenda kubwa kutoka serikalini, wanavyozipata wanajua wao. Kinachotushangaza kila mmoja anasema atamuanika mwenzake,” alisema mfanyabiashara huyo aliyeomba jina lake lisitajwe.
Taarifa za ndani kutoka kwa watu walio karibu na Manji, zinadai kuwa mfanyabiashara huyo hakufurahishwa na jinsi mchakato wa upatikanaji zabuni hiyo ulivyoendeshwa, na sasa anakusudia kuvujisha katika vyombo vya habari taratibu zilizokiukwa katika mchakato wa utoaji wa zabuni hiyo.
Zinadai kuwa, Manji anajiandaa kuweka wazi jinsi sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 ilivyokiukwa wakati wa mchakato wa utoaji zabuni hiyo.
Katika mradi huo, Jeetu ambaye anatajwa kuwa mwakilishi wa Kampuni ya Escort hapa nchini, yenye makao makuu yake nchini India, ambayo imeshinda zabuni hiyo, anadaiwa kuwashawishi maofisa wa juu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo limekabidhiwa jukumu la kuutekeleza mradi huo na serikali, kuipatia kampuni hiyo.
Habari hizo zimedai kuwa, Jeetu alifanikisha mpango huo baada ya kuwaunganisha maofisa kadhaa wa ngazi za juu wa JKT na watendaji wakuu wa Escort walioko India, ambao baada ya kuhakikishiwa kupewa zabuni hiyo, waliwaalika maofisa kadhaa wa JKT kwenda nchini humo kwa ajili ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa kazi ya kusambaza matrekta hapa nchini.
Taarifa zaidi zilidai kuwa, tayari baadhi ya viongozi wa juu wa JKT wamekwisha safiri hadi India kusaini mkataba huo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa, Manji anapinga hatua ya viongozi wa JKT kwenda kusaini mkataba huo nchini India, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watendaji wa serikali wamekwishalalamikiwa kwa kusaini mikataba inayohusu miradi ya kitaifa nje ya nchi.
Aidha, inadaiwa kuwa, baadhi ya habari zinazotarajiwa kusambazwa zitakuwa zinahoji ukiukwaji wa taratibu kwa kutoa zabuni hiyo pasipo kuitangaza kama sheria ya manunuzi ya umma inavyoelekeza, licha ya Baraza la Mawaziri kuujadili mradi huo na kutoa baraka kwa JKT kuutekeleza.
Kwa upande wa Jeetu, taarifa zinadai kuwa, anajiandaa kujibu tuhuma za aina yoyote zitakazotolewa katika vyombo vya habari, zikiwa na lengo la kuichafua Kampuni ya Escort au zinazohusu upatikanaji wa zabuni hiyo.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu serikalini aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake alieleza kuwa, anafahamu kuwa Serikali ya India ilitoa mkopo usiokuwa na riba, wa zaidi ya sh bilioni 50 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kununulia matrekta, wakati Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alipofanya ziara nchini humo mapema mwaka huu, kwa sharti la kulipwa katika kipindi cha miaka 10.
Alisema sharti jingine lililotolewa katika kutoa mkopo huo, linaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha inanunua matrekta hayo kutoka kampuni za India na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema, serikali iliamua kuikabidhi JKT jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuondoa mazingira yoyote ya kutokea udanganyifu katika kuutekeleza.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake iwapo kuna taarifa za baadhi ya maofisa wa JKT waliokabidhiwa jukumu la kusimamia utekelezaji huo, kuzungumza na mwakilishi wa Kampuni ya Escort hapa nchini (Jeetu), kisha wakaipa kampuni anayoiwakilisha zabuni hiyo bila kufuata taratibu.
“Hili jambo linaweza kuharibu kabisa sifa ya JKT kama litakuwa kweli, kwa sababu itakuwa ni kashfa kubwa kwa jeshi kukiuka taratibu za manunuzi ya umma. Ingawa kuna imani kuwa si rahisi mambo ya kijeshi kuchunguzwa, lakini hili liko wazi mno kwa sababu ni zabuni iliyo wazi iliyokuwa ikifuatiliwa na wafanyabiashara wengi, hivyo hao hao wanaweza kuwa wametoa siri za taratibu kukiukwa,” alisema ofisa huyo.
No comments:
Post a Comment