MALUMBANO makali yameendelea kuitikisa Kamati ya rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi baada ya makombora ya juzi kuelekezwa kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango na mumewe, mzee John Malecela.
Kamati hiyo imekuwa ikipokea mashambulizi makali baina ya wabunge ambao wanaonekana kuwa vinara wa vita dhidi ya ufisadi na wale ambao wanaona kuwa vita hiyo inawalenga, kiasi cha kurushiana tuhuma nzito zilizo na mwelekeo wa kuchafuana.
Baada ya kulipuana Jumanne, juzi ilikuwa zamu ya Mama Kilango na mumewe Malecela wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba alipotoa tuhuma nzito akidai kuwa wawili hao pia wamekula fedha za ufisadi.
Habari kutoka vyanzo vyetu zilieleza kuwa Simba alidiriki kudai kuwa hata harusi ya makamu huyo wa zamani wa CCM na Kilango ilifadhiliwa na mtuhumiwa wa ufisadi, Jeetu Patel.
Patel kwa sasa ana kesi katika Mahakama ya Kisutu akituhumiwa kuiibia Benki Kuu (BoT) kwa kuchota takribani Sh11 bilioni kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Akijieleza kwenye kamati hiyo, Simba alimtuhumu Malecela, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza, kuwa wakati akiwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2005, Jeetu Patel alimpa Sh200 milioni kwa ajili ya kampeni zake.
Malecela, ambaye wakati huo alikuwa makamu mwenyekiti wa CCM, aliondolewa mapema kwenye mbio za urais, ikiwa ni mara ya pili baada ya kuenguliwa tena mapema mwaka 1995.
Waziri huyo mwenye dhamana ya utawala bora akiwa na taasisi nyeti kama Takukuru na Idara ya Usalama wa Taifa, alizidi kurusha makombora kwa wanandoa hao, akisema Mama Kilango ni mnafiki na sio msafi kiasi cha kuwanyooshea wengine vidole wakati harusi na kampeni zake za ubunge zilifadhiliwa na mtuhumiwa huyo wa ufisadi.
Habari zinasema kuwa Mama Simba alikuwa akizungumza kwa kujiamini na kwa ujasiri na kumtuhumu Mama Kilango kuwa kelele zake zote zinatokana na nongwa ya “kuukosa U-first lady (kuwa mke wa rais).
Alieleza kuwa kelele zote za mbunge huyo wa Same Mashariki zinatokana na chuki na uchu wa madaraka na si kweli kwamba ni mpinga ufisadi, kwa mujibu wa mtoaji habari wetu.
Lakini Patel, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo za Waziri Simba kwamba alifadhili harusi ya Malecela na kampeni zake za urais, alionekana kustuka na kusema: "Haa...we nani kakwambia... Bwana ehee, mimi sijui lolote kuhusu hayo.
"Kwa sasa mimi najiangalia mwenyewe, nina matatizo yangu mengi nahangaika nayo."
Hata alipofafanuliwa kwamba, maneno hayo yalisemwa na Waziri Simba, alijibu: "Kama wao wamesema wenyewe huko, mimi sijui."
Naye Kilango alisema alishuhudia wakati wakati makombora hayo yakirushwa na kueleza kwamba anajiandaa kujibu mapigo.
Mbunge huyo machachari alisema anajua kwamba mambo yote yaliyosemwa, yanamlenga yeye na si mumewe Malecela.
"Mimi ni mwanasiasa... andikeni yote yaliyozungumzwa bila ya kuacha baadhi na siwezi kuwashtaki," alisema Kilango.
Mzee Malecela hakutaka kuzungumzia lolote kuhusu tuhuma hizo wakati alipoulizwa juu ya uhusiano wake na Patel na kama aliwahi kupokea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kampeni.
"Ahaa... kijana naomba uniache nipumzike," alisema Malecela.
Mbali na mzee Malecela na mkewe, Waziri Simba pia alimgeukia mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi akimtuhumu kuwa anaendesha vyombo vya habari vinavyoichafua CCM na serikali yake kwa maslahi yake binafsi.
Pia alimshambulia mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe na mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, akiwatuhumu kuwa ni watu wenye njaa na kwamba, wanalipwa fedha kufanya kazi hiyo.
Waziri Simba alisema kuwa hata tuhuma dhidi ya mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, zimetokana na chuki binafsi.
Simba alisema kuwa uchunguzi wa kashfa ya rada ulishamalizika na Chenge akasafishwa na kuongeza kwamba hata uchunguzi wa Richmond umebaini kulikuwa hakuna rushwa, kwa mujibu wa mtoaji habari wetu.
Suala la Richmond liliibuka tena mbele ya kamati hiyo ya Mwinyi wakati mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi alipolalamika kuwa ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyoozwa Dk Mwakyembe haikumtendea haki.
habari hizo toka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Karamagi alisema ripoti ya Richmond ilionea baadhi ya watu na akapendekeza iundwe tume huru kupitia mchakato huo kuona kama wana makosa ili haki itendeke.
Mbunge huyo ambaye alijiuzulu uwaziri baada ya Lowassa kuachia wadhifa wake wa waziri mkuu kutokana na kashfa hiyo, alisema maamuzi yake kuhusu Richmond yalitokana na mapendekezo ya Bodi ya Tanesco.
Naye Dk Mwakyembe alijibu hoja iliyotolewa Jumanne na mbunge wa Ukonga, Dk Makongoro Mahanga aliyedai kuwa ripoti ya Richmond ni 'feki', akisema tatizo la Dk Mahanga ni uelewa mdogo.
Kuhusu hoja ya Karamagi, Dk Mwakyembe alisema malalamiko yake si sahihi kwa sababu yapo maeneo mengi ambayo Karamagi alishiriki na yako bayana hayahitaji mjadala.
Aliwatahadharisha Wabunge kuacha kudodosa sana ripoti ya Richmond kwani watazidi kumchafua Lowassa na kwamba wanaweza kufungwa kwa sababu upo ushahidi dhahiri.
Dk Mwakyembe aliwataka viongozi wa CCM wenye tuhuma kuiga mfano wa Mzee Mwinyi aliyejiuzulu baada ya mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola mkoani Shinyanga.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, alimshambulia spika wa Bunge, Samuel Sitta akidai kuwa kama si mizengwe, suala la Richmond lingemalizwa kwa taratibu za kichama.
Habari hizo zinadai kuwa Chenge, aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, alisema Lowassa alizungukwa na kwamba kulikuwa na njama za kummaliza ingawa hakusema njama hizo zilifanywa na nani.
Chenge aliitetea serikali ya awamu ya tatu kuhusu kuingia mikataba mibovu na kusisitiza hakukuwa na uzembe kwani mikataba yote ilipitiwa na kukubaliwa na Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo, mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi alisimama na kuomba kutoa taarifa na kumwomba Mzee Mwinyi na kamati yake wawabane wabunge wanaodai wanasema ukweli.
Masilingi alipinga maelezo ya Chenge kuhusu mikataba na kusisitiza kuwa maelezo yake yalijaa ushabiki na kusema Baraza la Mawaziri liliridhia mikataba kutokana na ushauri wake (Chenge).
Mbunge wa Kwela, Dk Chrisant Mzindakaya, ambaye aliwahi kupata umaarufu kwa kulipua kashfa, aliwataka wabunge wakubali matokeo kuhusu Ripoti ya Richmond ili taifa lisonge mbele badala ya malumbano yasiyokwisha.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Mzindakaya aliwataka wabunge wafahamu kuwa ripoti hiyo ilishapitishwa na Bunge na haiwezi kurejeshwa ianze tena upya.
Naye Dk Mlingwa (Shinyanga Mjini), alisema mpasuko unaoinyemelea CCM unatokana na chama hicho kuacha misingi yake ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi na badala yake kinawakumbatia wafanyabiashara.
Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Emanuel Nchimbi alitumia nafasi yake kuomba maridhiano ya wabunge wa CCM, kujenga moyo wa kusameheana ili chama kisonge mbele.
No comments:
Post a Comment