.

.

.

.

Friday, November 13, 2009

SIMANZI WILAYANI SAME

SIMANZI na vilio jana vilitawala kwenye mazishi ya watu 2O waliofariki dunia kwa kufunikwa na kifusi kilichoporomoka mlimani na kufukia nyumba zao usiku wa manane katika Kata ya Mamba Miamba, wilayani Same, Kilimajaro.
watu zaidi ya 1,000 waliokusanyika katika msiba huo mkubwa wakiwa wamefunikwa na simazi, huku wakilia kwa uchungu kutokana na kupoteza ndugu zao katika mkasa huo wa kutisha.
Asilimia kubwa ya watu walionyesha masikitiko yao, hasa kwa familia ambayo imepoteza watu 15 na kati ya hao wanne hawajapatikana mpaka sasa.
Wanachi hao waliiomba serikali iwasaidie kutafuta miili ya watu hao na ikiwezekana watumie kikosi cha mbwa ili kubaini mahali ilipo.
Elineema Shambi, mmoja wa ndugu wa wanafamilia 15 waliofariki dunia na ambaye alinusurika kwa vile alikuwa amekwenda mjini Moshi kwa shughuli za kibiashara, alisema kwa majonzi kwamba amepoteza mke na watoto wake wanne ambao walifukiwa na kifusi hicho.
Alisema alikwenda mjini Moshi kununua bidhaa za kuuza, na kesho yake asubuhi alipigiwa simu na kuondoka mara moja. Alieleza kuwa alipofika alikuta nyumba yake imefunikwa kabisa kiasi cha kutoonyesha kama kulikuwa na nyumba na mwili wa mkewe ulikuwa haujapatikana hivyo akasaidia kuutafuta na kuupata pamoja na miili ya watoto wake.
Alifahamisha kuwa yeye ni mmoja kati ya ndugu wa watu 15 waliofariki katika tukio hilo la kutisha.
Akisimulia juu ya maporomoko hayo, alisema, dalili za mlima huo kuporomoka zilianza kuoneka mwaka jana kwa kuwa kulikuwa na ufa, hata hivyo hakueleza kwamba ni kwa nini hawakuhama katika eneo.
Akiunga mkono maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega alibainisha kuwa wananchi wa Kata ya Mamba Miamba walishaona dalili za kuporomoka kwa mlima ulioua watu 20, tangu mwaka jana, lakini hawakuchukua tahadhari.
Wakati Mbega akisema hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema haikuweza kutoa taarifa ya kutahadharisha wananchi dhidi ya janga hilo kwa kuwa vipimo vyake havikuweza kutabiri mvua kubwa.
Mbega alitoa kauli hiyo jana katika eneo hilo la maafa wakati akiongoza maelfu kwa mamia ya wananchi wa eneo hilo na kutoka nje ya Wilaya ya Same katika mazishi ya watu waliofariki kutokana na janga hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mlima huo ulianza kuonyesha ufa mwaka jana na baadaye Mei mwaka huu ufa huo ukazibika, lakini kumbe ndani ya mlima bado ulikuwa umeacha shimo kubwa.
Kwa mujibu wa Mbega, ambaye pia ni mbunge wa Iringa Mjini, pamoja na dalili zote hizo wananchi hao hawakuchukua hatua za tahadhari ikiwamo kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika ikiwamo serikali.
RC Mbega alisema endapo wananchi wangetoa taarifa mapema, serikali ingeweza kutuma wataalamu wake ambao wangesaidia kushauri jinsi ya kuepuka janga hilo.
Hadi kufikia jana saa 9:00 alasiri, miili ya watu wazima 19 na mtoto mchanga wa miezi tisa ilikuwa imeopolewa kutoka katika vifusi vilivyoporomoka kwenye mlima huo wenye majabali makubwa ya mawe.
Madaktari walilazimika kufanya upasuaji kwenye maiti ya mwanamke aliyejulikana kama Wemael Mhina, 30, ambaye ingawa siku zake za kujifungua zilikuwa zimeshatimia, hakujifungua hadi alipofikwa na mauti hayo.
Mkuu wa mkoa alisema Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, Steven Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia, Maua Daftari wametuma salamu za rambirambi.
Katika kuungana na wafiwa katika msiba huo mkubwa, Mbega alisema serikali imetoa Sh2 milioni za rambirambi kwa wafiwa na kugharamia shughuli zote za mazishi, ikiwa ni pamoja na chakula, malazi, matibabu na majeneza.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa ameiomba serikali kutuma wataalamu wa miamba katika maeneo ya wilaya hiyo ili kuchunguza uhimili wake hasa kutokana na mvua nyingi zinazoendelea.
Marwa alisema tukio la kuporomoka kwa mlima liliwahi kutokea katika eneo la Hedaru, lakini halikusababisha madhara hivyo akasema upo umuhimu wa uchunguzi kufanyika.
Pia mkuu huyo wa wilaya aliuomba uongozi wa serikali na Jeshi la Polisi kutuma kikosi chake cha mbwa ili kusaidia kazi ya kutafuta miili ya watu wanne ambao wanaaminika bado wamenasa chini ya kifusi cha tope.
Marwa alisema mbwa hao watakuwa msaada mkubwa wa kubaini sehemu ambazo watakuwa wamefukiwa watu hao kutokana na mbwa hao kuwa na utaalamu na ujuzi wa kubaini mambo ya namna hiyo kwa kunusa.
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Mathayo David ambaye pia ni mbunge wa Same Magharibi, alisema msiba huo ni mkubwa na kwamba umemgusa.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Kilimanjaro isipokuwa Wilaya ya Siha, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya jirani,viongozi wa dini na wananchi.
Wakati wa mazishi hayo, kitongoji hicho cha Manja kilizizima kwa vilio na kwikwi kutokana na ukweli kuwa wengi waliofariki ni ndugu wa familia moja huku familia moja ikipoteza baba, mama na watoto wanne.
Eneo moja la makaburi kumezikwa ndugu tisa wa familia ambao walipoteza maisha katika tukio, wakati eneo jingine wamezikwa ndugu tisa wa familia moja huku eneo jingine wakizikwa ndugu wanne wa familia moja.
Shughuli za mazishi hayo zilianza saa 8:00 mchana na saa 9:15 alasiri ndipo waombolezaji walipoanza kazi rasmi ya kuzika huku simanzi kubwa ikionekana dhahiri miongoni mwa waombolezaji.
Wakati huohuo, Makoba Hassan na Thomas Ludovick wanaripoti kuwa TMA imesema haikuweza kuitahadharisha jamii kuhusu maafa yaliyotokea wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa sababu ya mvua kwa kuwa vipimo vyake havikuweza kutabiri.
Kaimu Mkurugenzi wa shughuli za utabiri nchini, Matitu Mohammed alisema jana ofisini kwake kuwa hali hiyo ilitokea kutokana na vipimo vyao vya utabiri wa hali ya hewa wilayani hapo kuwa mbali na eneo lililotokea tukio hilo.
"Tukio lilitokea sehemu za milimani ambako vipimo vyetu vya utabiri vilishindwa kurekodi na kutoa taarifa kwa watu wa eneo hili kutokana na kituo chetu kuwa mbali," alisema Mohammed.
Alisema dhana kuwa mvua hizo ni El-Nino si ya kweli bali mvua hizo kitaalamu zinaitwa mvua za vuli ambazo hutokea katika kipindi hiki na husababishwa na ongezeko la joto katika Bahari ya Pacific
"Naomba wananchi waelewe kuwa hakuna mvua za El-Nino bali ni mvua za vuli ambazo huambatana na mfumo wa pepo zinazovuma kutoka Bahari ya Pacific kuelekea Bahari ya Hindi hivyo kusababisha mvua kubwa kutokea katika maeneo yote duniani," alisema.
Alizitaja sehemu zilizowahi kutokea maafa katika kipindi kilichopita kuwa ni Hedaru, Makanya, katikati ya Same na Mwanga na Same yenyewe kwa sasa ikiwa ni mara ya pili.

No comments:

Post a Comment