.

.

.

.

Monday, December 21, 2009

SLAA ATUPA BOMU JINGINE

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, jana alifichua ufisadi mkubwa uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuingiza magari 200 aina ya Land Cruiser ‘mkonga’ bila ya kulipia sh milioni 600 za ushuru wa forodha kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Dk. Slaa aliyasema hayo jana katika mkutano mkubwa wa hadhara wa muendelezo wa Operesheni Sangara uliofanyika katika Kijiji cha Kilole wilayani Korogwe. Alisema amepokea taarifa hiyo jana kutoka kwa msiri wake ndani ya TRA.
Alisema hana ugomvi na CCM kuingiza magari 200 kwa ajili ya kupata ushindi mwaka 2010, lakini ugomvi wake mkubwa ni chama hicho kutoyalipia magari hayo ushuru wa sh milioni 600 ambazo zingewasaidia Watanzania katika kujenga nchi kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kwa kujiamini, alisema suala hilo lina ukweli usiokanushika. Alimtaka na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kama anaweza akanushe.
“Taarifa hii nimeipata leo, na ina ukweli ndani yake. Hivi ninavyoongea yanaweza kutolewa muda wowote bandarini. Kama suala hili ni uongo, Pinda akanushe. Na wakilipa leo waandike tarehe risiti ya leo kwa kuwa hadi ninavyoongea hayajalipiwa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema huo ni ufisadi mkubwa ambao unafanywa na CCM wakati vyama vingine vinalipa ushuru.
Dk. Slaa alisema kuwa mwaka 2005 CCM ilifanya ufisadi kama huo kwa kumtumia mfanyabishara mwenye asili ya Kiasia, Jeetu Patel, na kufanikiwa kuingiza magari 235 bila kulipia ushuru pia.
Alisema viongozi wote wa CCM wamewekana katika nafasi za uongozi, ndiyo sababu maadili katika nafasi za uongozi wa kiserikali na taasisi zake yamemong’onyoka.

No comments:

Post a Comment