TANZANIA imepanda chati kwa nafasi nane katika viwango vya ubora wa soka kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa .
Matokeo mazuri ya Kilimanjaro Stars iliyotwaa Kombe la Chalenji Jumapili kwa kuilaza Ivory Coast kwa bao 1-0 na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya The Cranes ya Uganda baada ya suluhu ya 0-0 kwenye nusu fainali ya michuano hiyo, ni sababu za kupanda kwake na kushika nafasi ya 116 kwa ubora duniani ikitokea nafasi ya 124 mwezi uliopita.
Kulingana na orodha hiyo iliyotangazwa jana na Fifa , Uganda ambayo bado ni kinara wa soka kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ingawa imeporomoka kwa nafasi 11.
Kwa mujibu wa orodha hiyo ya Fifa, Tanzania imepanda katika viwango hivyo vipya baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya Chalenji ambayo yanatambuliwa na Fifa kama mechi za kirafiki za kimataifa.
Katika mashindano hayo ya Chalenji , Kili Stars yaTanzania Bara ilizifunga Rwanda 1-0, Burundi 2-0, Somalia 3-0, Uganda 5-4 kwa penalti na Kenya 1-0 wakati wa maandalizi ya mashindano hayo.
Kwa kupanda kwa nafasi nane Tanzania inashika nafasi ya pili katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati huku ikizidiwa na Uganda ambayo inashika nafasi ya 80 katika viwango vipya vya Fifa ikiwa imeshuka kwa nafasi 11.
Kenya inashika nafasi ya 120 ikiwa imeshuka kwa nafasi nne, hivyo kuwa ya tatu katika ukanda huo wa Afrika ya Mashariki ikifuatiwa na Burundi katika nafasi ya 128 ambayo imepanda kwa nafasi nane na Rwanda katika nafasi ya 132 ambayo imeshuka kwa nafasi tano.
Orodha hiyo pia inaonyesha nchi za Afrika ya Magharibi na Kaskazini zimeendelea kufanya vizuri kuzidi nchi za Afrika ya Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika.
Nigeria ambayo timu yake ya wanawake ilitwaa ubingwa barani humo inashika nafasi ya 32, Algeria ipo nafasi ya 35, Cameroon nafasi ya 37, Gabon nafasi ya 39, Tunisia ni ya 45, Guinea nafasi ya 46, wakati Afrika Kusini ipo nafasi ya 51, Botswana nafasi ya 53, Zambia 76, Malawi 86 na Angola 88.
Mabingwa wa dunia Hispania wameendelea kushika namba moja katika orodha hiyo huku wakifuatiwa na Uholanzi katika nafasi ya pili, nafasi ya tatu inashikiliwa na Ujerumani na Brazil ipo katika nafasi ya nne.
Nchi inayoshika mkia ni Papua New Guinea ambayo inashika nafasi ya 203.
Katika viwango vya Fifa mwaka huu, Tanzania imekuwa ikipanda na kushuka kwani mwezi Januari ilikuwa nafasi ya 108, Februari nafasi ya 108, Machi ikawa ya 109, Aprili ikashika nafasi ya 108, Mei ikabakia katika nafasi ya 108, Juni nafasi ya 112, Julai 111, Agosti 111, Septemba 120, Oktoba 124 na Novemba - Desemba nafasi ya 116.
Mwezi Februari mwaka 1995, Tanzania ilishika nafasi ya 65 ambacho ndicho kiwango cha juu kabisa ambacho iliwahi kushika, kiwango cha chini kabisa kwake (Tanzania) kuwahi kushika ni nafasi ya 175 ambapo nafasi hiyo hiyo ilikuwa Oktoba 2005.
No comments:
Post a Comment