Haikuwa kazi rahisi kwa Kili Stars kufikia hatua hiyo ambayo inamaanisha kuwa imeivua ubingwa Uganda Cranes ambayo ilikuwa ikijaribu kulitwaa kombe hilo kwa mwaka wa tatu.
Matokeo hayo pia ni pigo kwa kocha wa Uganda, Bobby Robinson raia wa Scotland ambaye amejiwekea rekodi ya kushinda mechi zote za michuano ya Chalenji tangu alipoanza kukinoa kikosi hicho miaka mitatu iliyopita.
Kili Stars ambayo ilianza vibaya michuano hiyo na kubadilika taratibu, iliuanza mchezo huo wa jana kwa kasi mbele ya mashabiki wake wengi kwa kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Uganda, lakini mhambuliaji wake pekee aliyechezeshwa mbele, Mrisho Ngassa akisaidiwa na John Boko walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Mikwaju 5-4 iliyoivusha Kili Stars ilijazwa wavuni na Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Shaaban Nditi, Machaku Salum na Erasto Nyoni.
Matokeo hayo yamedumisha rekodi ya Tanzania dhidi ya Uganda katika michuano hiyo, ambako zimekutana mara nne katika nusu fainali na mshindi kupatikana kwa penalti, huku Kili Stars ikishinda mara tatu.
Zilianza kukutana mwaka 1979, ambako Tanzania ilishinda 5-3, zikacheza tena mwaka 1990 ambako Uganda ilishinda 6-5, mwaka 1994, Tanzania ikashinda 4-3.
Kipa Juma Kaseja aliibuka shujaa kwa kuokoa mkwaju wa Tonny Mawejje.
Katika dakika 120 za mchezo huo wa nusu fainali, timu zote zilicheza kwa kushambuliana na kukosa nafasi, zikiwamo za wazi.
Stars walianza kukosa bao kupitia kwa Mrisho Ngassa ambaye shuti lake liligonga nyavu alipounganisha moja kwa moja pasi ndefu ya Nsajigwa dakika ya 27, kabla ya nahodha huyo kuipenya tena ngome ya Uganda Cranes na kupiga shuti lililokwenda nje.
Cranes ambao nahodha wao, Andrew Mwesigwa alikuwa ameapa kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu walijibu mapigo kwa kufanya mashambulizi ya kushitukiza golini kwa Kili Stars kupitia kwa Massa Simeon na Mike Serumanga, lakini kipa Kaseja na ngome yake iliyokuwa chini ya Juma Nyoso, Kelvin Yondani ilikuwa makini kuokoa hatari zote.
Nahodha Nsajigwa ambaye alicheza vizuri jana alionyeshwa kadi ya njano dakika 19, kwa kumchezea vibaya Godfrey Walasumbi.
Nao Idrissa Rajabu, Nditi na Emmanuel Okwi wa Uganda Cranes walishuhudia wakilimwa kadi na mwamuzi ambaye pia ni mhandisi kijana Davies Omweno, 26 kutoka Kenya kwa nyakati tofauti.
Dakika 120 hazikuwa za mzaha baada ya mwamuzi huyo kusimamisha mpira wakati wa dakika za nyongeza kwenda nje ya uwanja kunywa maji baada ya kuzidiwa na joto na kasi ya mchezo.
Kocha Jan Poulsen aliwapumzisha Rajabu, Jabir Aziz na John Boko na kuwaingiza Salum Machaku, Erasto Nyoni na Gaudence Mwaikimba.
Mwenzake Robinson wa Uganda aliwapumzisha Steve Bengo na nafasi yake kuchukuliwa na Robert Ssentongo , pia alimtoa Mike Serumaga na kuingia Derick Walulya.
Awali, Tembo watoto wa Ivory Coast walikata tiketi ya kucheza fainali dhidi ya Kili Stars baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi mabingwa mara nne, Ethiopia.
Mshambuliaji Kipre Tchetche aliyeingia kipindi cha pili aliwazidi mbio mabeki wa Ethiopia, kupokea krosi ya pacha wake, Kipre Bolou na kupiga shuti lilokwenda pembeni na kumwacha kipa asijue kwenye dakika ya 71.
Tchetche nusura afunge bao la pili kuunganisha vizuri krosi fupi, lakini shuti lake liligonga mwamba na kutoka nje. Katika mchezo huo timu zote zilionyesha soka ya nguvu na umahiri mkubwa.
Kocha wa Ethiopia, Onuora Ifem, maarufu Iffy ambaye ni mzaliwa wa Scotland mwenye asili ya Nigeria alisema mchezo ulikuwa wazi kwa timu zote wao walipata nafasi wakashindwa kuzitumia.
Naye Kouadio Geogres wa Ivory Coast alisema mabadiliko aliyofanya ndiyo yaliyompa ushindi na kumwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma.
"Nimekuja kutwaa ubingwa hapa, nawashukuru vijana wangu kwa kucheza soka ya nguvu na kufanikiwa kufika katika hatua ya fainali."
Kikosi cha Kili Stars kilikuwa:
Juma Kaseja, Shadrack Nsajingwa, Stephano Mwasika, Kelvin Yondani, Juma Nyoso, Shabani Nditi, Nurdin Bakari, Jabir Azizi, Mrisho Ngassa, Jonh Boko na Idrisa Rajabu.
Uganda Cranes
Odongkara Robert, Massa Simeon, Isinde Isaac, Walusimbi Godfrey, Mwesingwa Andrew, Mudde Musa, Danny Wagaluka, Maweje Tony, Kiseka Henry, Robert Ssentongo na Steven Bengo.
No comments:
Post a Comment