- Katika jamii nyingi za Kiafrika wanawake walitegemewa kuolewa mara tu walipovunja ungo. Binti ambaye alibakia kuwa nyumbani bila kuolewa alionwa kama mwenye matatizo na kwa kawaida halikuwa jambo jema. Hata mwanamke angekuwa amesoma vipi, hata kama angekuwa na kazi nzuri au uwezo mkubwa wa kiuchumi kiasi cha kuweza kuendesha maisha yake bila kumtegemea mwanaume, bado jamii ilimtegemea aolewe.
- Katika gazeti moja la leo kulikuwa na makala iliyokuwa, mbali na mambo mengine, inaonyesha jinsi ambavyo idadi ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na kuendelea ambao hawajawahi/hawataki kuolewa imekuwa ikingezeka hapa Marekani. Kwa mfano makala hiyo imebainisha kwamba mwaka 2006 asilimia 27.3 ya wanawake wote hapa Marekani walikuwa hawajaolewa na hawategemei kuolewa. Mwaka 2008 idadi hiyo ilikuwa imefikia zaidi ya asilimia 28.1%. Wanawake wengi wanasema kwamba hawaoni sababu ya kuolewa.
- Kwa vile hizi ni zama za utandawazi - ambapo tunaiga kila kitu cha wazungu, sitashangaa kama jambo hili tutaliiga pia. Hata hivyo nadhani kwamba pengine uigaji wetu hapa utachukua muda kwani nimeambiwa kwamba sasa kuoza mtoto pale Dar es salaam imegeuka kuwa ni nafasi ya wazazi kujionyesha uwezo wao wa kifedha kuanzia kitchen party, send off party (sijui kama hizi ni tofauti) na hatimaye harusi yenyewe. Wazazi wanatumia mamilioni ya shilingi katika shughuli hizi za kuoza watoto wao na pengine kila binti atapenda siku moja kushiriki katika umeremetaji huu wa kitambo na kuwafurahisha wazazi wake. Naamini pia kwamba jamii bado inaiona ndoa kama taasisi muhimu katika ujenzi na utangamano wa jamii. Swali hasa ambalo ningependa kuwauliza wanawake ni hili: Je, kuolewa ni lazima? Kwa nini?
- Ati, jamii ya leo inamtazamaje mwanamke ambaye ameamua kukaa peke yake bila kuolewa?
SOURCE : MATONDO
No comments:
Post a Comment