.

.

.

.

Tuesday, March 01, 2011

RAIS JK ATEUA MAKATIBU WAKUU WAPYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu watano wapya na kuwahamisha wengine wanne kutoka wizara moja kwenda nyingine. Uteuzi na uhamisho huo unaanza mara moja.

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Februari 28, 2011, mjini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Ndugu Phillemon L. Luhanjo inasema kuwa mabadiliko hayo yanatokana na Muundo mpya wa Serikali ambako Wizara ya Miundombinu imegawanywa katika wizara mbili, na baadhi ya Makatibu Wakuu kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amemteua Bw. Fanuel E. Mbonde kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi wake Bw. Mbonde alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wengine walioteuliwa ni B. Hussein A. Kattanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Bw. John M. Haule kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Bw. Herbert E. Mrango kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi; na Bw. Eric K. Shitindi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira.

Kabla ya uteuzi wake Bw. Kattanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Bw. Haule alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha; Bw. Mrango alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Bw. Shittindi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kuhusu uhamisho, Rais Kikwete amemhamisha Bw. Sazi B. Salula kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais; Bibi Maimuna K. Tarishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii; Injinia Omar A. Chambo kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi akitokea Ukatibu Mkuu wa Wizara ya zamani ya Miundombinu; na Bibi Kijakazi R. Mtengwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Taarifa hiyo ya Ndugu Luhanjo imesema vile vile kuwa Dkt. Ladislaus C. Komba, aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anapangiwa kazi maalum katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamishia Bibi Elizabeth J Nyambibo Wizara ya Fedha na Uchumi ambako anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na Bwana John H. Haule. Kabla ya uhamisho wake, Bibi Nyambibo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Taarifa hiyo ya Ndugu Luhanjo imesema kuwa Makatibu Wakuu wapya wataapishwa saa tatu asubuhi leo, Machi Mosi, 2011.

Mwisho.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Februari, 2011

No comments:

Post a Comment