.

.

.

.

Saturday, January 28, 2012

WAZIRI MKUU AKUTANA NA RAIS JK

RAIS Jakaya Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na kufanya mazungumzo, huku kiongozi huyo wa Uingereza akisifia Tanzania kwa kupiga hatua katika sekta ya elimu na kilimo. 


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na kusainiwa na  Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premiere Kibanga, Cameron alimweleza Rais Kikwete kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta za kilimo na elimu barani Afrika. 


“Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ametoa pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yao jana (juzi) jioni hapa Davos, ambapo wote wawili wanahudhuria mkutano wa uchumi duniani wa kila mwaka, World Economic Forum (WEF),” inaeleza taarifa hiyo. Inasema katika mkutano huo masuala ya uchumi, ikiwamo athari zinazokabili uchumi duniani kwa sasa na jitihada mbalimbali zinazofanywa kuunusuru vitajadiliwa.


 “Afrika inapitia kipindi cha mabadiliko ambayo ni chanya, Tanzania ni mfano bora wa kuigwa katika hili,” taarifa hiyo ilimnukuu Cameron akimweleza Rais Kikwete walipokutana juzi jioni. Inasema katika mazungumzo yao, Rais Kikwete amemweleza Cameron kuwa kilimo ni sekta kubwa na inayotegemewa na Watanzania wengi na kwamba, Serikali inalenga kujitosheleza kwa chakula ndani na nje ya nchi. 


Inasema Rais Kikwete na Cameron pia walizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu siasa na usalama barani Afrika. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, awali juzi asubuhi, Rais Kikwete alijumuika na viongozi wengine kutoka Ethiopia, Guinea-Conackry, Kenya na Afrika Kusini  kuzungumzia mabadiliko mbalimbali ya uchumi na maendeleo barani Afrika. 


Taarifa hiyo inaeleza kuwa, mjadala huo uliongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown, ambapo Rais Kikwete alisema bara la Afrika limepata athari mbalimbali zinazotokana na  mabadiliko ya uchumi duniani. “Afrika ina mahitaji zaidi katika kutekeleza sera zinazolenga uchumi imara na kuwekeza katika sekta za elimu, utafiti, kilimo, viwanda na miundombinu,” taarifa inamkariri Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment