Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda akilia na kufarijiwa.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda amejikuta akiangua kilio kwa uchungu mbele ya wanaharakati ambao walimtembelea mwanae, Dk. Steven Ulimboka kumpa pole kufuatia tukio la kutekwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana.
Hali hiyo ilitokea jana jioni katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo wanaharakati kutoka taasisi na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu walifika kwa lengo la kumpa pole Dk. Ulimboka kufuatia kitendo kilichomfika.
Mzee Mwaitenda alijikuta akibubujikwa na machozi na kushindwa kuendelea kuzungumza alipokuwa akitoa shukrani kwa wanaharakati hao, kwa niaba ya mwanaye ambaye wanaharakati hao walishindwa kumuona wote kutokana na hali yake ilivyo sasa.
“Niseme wazi nimefarijika sana kwa ujio wenu kumwona mwanangu dhidi ya mambo ya kikatili aliyofanyiwa akitetea haki za wengine…,” alisema mzee Mwaitenda kabla ya kushindwa kuendelea na kuangua kilio mbele ya wanaharakati.
Baada ya tukio hilo baadhi ya wanaharakati walimshika wakishirikiana na wanafamilia ya mzee Mwaitenda na kumbebeleza kisha kumtoa mbele ya mkusanyiko huo wa wanaharakati na kumrudisha wodini huku wakimfariji.
Wakizungumza mara baada ya tukio hilo wanaharakati wameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyoendelea MOI eneo ambalo amelazwa kiongozi huyo wa madaktari ambavyo vimeendelea kutishia usalama wa Dk. Ulimboka.
Akifafanua zaidi mwakilishi wa wanaharakati hao, Markos Albania alisema taarifa walizozipata usiku wa juzi kuna wagonjwa ‘feki’ ambao walijitokeza MOI huku wakitaka kulazwa wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) alipolazwa Dk. Ulimboka lakini baadaye waligoma kuingizwa wodini.
“Wapo wagonjwa ambao waliletwa na kutaka kupelekwa ICU moja kwa moja…kuna watu wanakuja usiku wa manane wakitaka kumtembelea Dk. Ulimboka…matendo yanayoendelea kutokea ukilinganisha na kauli za Serikali zilizotolewa bungeni yanatishia usalama na uhai wa mgonjwa,” alisema Albania.
Aidha amesema kitendo cha vyombo vya usalama kuendelea kumuhoji Dk. Ulimboka akiwa hoi hospitalini si vya kiungwana kwani tayari muhusika amewataja hadi kwa majina watu ambao anawashuku lakini hadi sasa hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hayo wanaharakati hao wameitaka Serikali kuunda tume huru mchanganyiko na raia ambayo itachunguza kiundani suala hilo, kwani hawana imani na Jeshi la Polisi ambalo limedai kuunda timu ambayo inachunguza kwa kina suala hilo.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa madaktari ambao wanaendelea na mgomo wan chi nzima kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao alitekwa juzi na watu wasiojulikana na kupigwa na kuteswa kikatili kabla ya kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
MUNGU ATATENDA YAKE NA HANA MPINZANI HIVYO ARUBAINI YA WAHUSIKA IKO MEZANI KWA MUNGU ENYI RAIA WEMA ONGEZENI SALA NA MAOMBI ILI MUONE MAJIBU YA MUNGU YASIVYO FICHA CHO CHOTE!
ReplyDelete