.

.

.

.

Wednesday, August 01, 2012

MH.LISSU ATOA MAJINA YA WABUNGE SABA WALA RUSHWA

Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu  ametaja majina ya  wabunge saba wa CCM kuhusika na tuhuma za ufisadi na kufanya  hali ya hewa bungeni kuchafuka baada ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kuomba mwongozo wa Spika kama anaweza kumshtaki mahakamani kwa madai kuwa amemdhalilisha.

Wakati Ole Sendeka akieleza kusudio lake hilo, Mbunge wa Viti Maalumu, Sara Msafiri ambaye Lissu alimtuhumu kufanya biashara ya matairi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kumhonga Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Eliakim Maswi, rushwa ya Sh50 milioni alisema anasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Ole Sendeka na Msafiri ni miongoni mwa wabunge saba wa CCM waliotajwa na Lissu juzi, kwamba wanalichafua Bunge kutokana na kujihusisha na mambo yenye mgongano wa kimasilahi
Wabunge wengine waliotajwa na Lissu ni Nasir Abdallah (Korogwe Mjini), Mariam Kisangi na Vicky Kamata (Viti Maalumu), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) na mbunge mmoja ambaye hatutamtaja kwa sababu hajapatikana kuzungumzia tuhuma zake.

Wabunge hao wote walishazungumzia tuhuma zaona kukanusha kuhusika. Lakini, jana Ole Sendeka baada ya kipindi cha maswali na majibu, aliomba mwongozo wa Spika kutaka ufafanuzi endapo kauli hizo za Lissu zina kinga ya Bunge ili aende mahakamani na kama hazina alitaka mwongozo wa Spika.
“Mheshimiwa Spika, jana Lissu aliitisha mkutano na waandishi wa habari na akanitaja mimi na wabunge wengine wa CCM kwamba ndiyo tunaohusika na tuhuma hizi za ufisadi. Sasa naomba mwongozo wako. Kauli hizo zina kinga ya Bunge au la ili niweze kwenda mahakamani,” alisema.

Katika mwongozo wake, Spika Makinda alisema kwa kuwa kauli hizo zilitolewa ndani ya maeneo ya Bunge zina kinga... “Ila napenda kuwaambia kuwa Bunge hili liwe na subira. Kuhusu aliyoyasema jana Lissu sisi tutamtaka yeye ndiye awe shahidi wa kwanza katika vikao vya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge. Atupe ushahidi tupate pa kuanzia.”

Kwa upande wake, Msafiri alisema ana imani kwamba kamati husika itatenda haki na kwamba yeyote anayemtuhumu apeleke ushahidi katika kamati hiyo.
"Siwezi kuzungumza kitu kwa sasa maana tuhuma ni tuhuma tu, mara huyu kasema hili mwingine kasema lile, kwa hiyo tusubiri tu matokeo ya Kamati ya Bunge na tumeambiwa inafanya kazi kwa kasi sana,” alisema Msafiri.

Msafiri pia anadaiwa kwenda kwa Maswi kumwomba radhi na kumsihi asitoe ushahidi dhidi yake mbele ya Kamati ya Bunge.

Habari kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini zimedai kuwa baada ya mjadala wa ufisadi kulipuka bungeni mwishoni mwa juma, mbunge huyo aliamua kuomba radhi kama njia ya kujinusuru na adhabu inayoweza kutolewa dhidi yake kama Bunge litathibitisha kuwa aliomba rushwa.

Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge namba 3 ya mwaka 1988, inataka Mbunge anayethibitika kutumika na watu kutoa michango au kuandika bungeni kwa masilahi ya mtu huyo ama kujihusisha mwenyewe katika masuala ya rushwa, afukuzwe ubunge na kufungwa kifungo cha miaka mitano.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mbunge huyo anadaiwa kufika Ofisi za Nishati na Madini zilizoko Mjini Dodoma Jumapili asubuhi, ikiwa ni siku moja baada ya Bunge kupitisha azma hiyo. Akaonana na Maswi na kuomba radhi katika kikao kilichowashirikisha watu watatu.

Habari zaidi zimeeleza kuwa lengo la mbunge huyo kuomba radhi ni kumshawishi katibu huyo ili asishirikiane na mamlaka zinazofuatilia tuhuma hizo ikiwamo Bunge katika kutoa taarifa kuhusu suala hilo.

Kuhusu suala hilo, Msafiri pia alisema anaiachia Kamati hiyo ya Bunge kufanya kazi yake.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipotakiwa kuzungumzia hatua ya mbunge huyo kuomba radhi, alisema asingependa kuzungumzia masuala ya watu, bali utendaji wa kazi katika wizara yake. 

Hata hivyo alieleza kuwa anachofahamu siku ya Jumapili, katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini Dodoma, kulikuwa na kazi ya watendaji wa wizara hiyo kuonana na wabunge.

No comments:

Post a Comment