.

.

.

.

Thursday, October 18, 2012

VURUGU KUBWA DAR NA ZANZIBAR ........ MABOMU YA MACHOZI YATUMIKA

Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar


POLISI mkoani Dar es Salaam na wale wa Kisiwani Zanzibar, jana walitumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kusambaratisha makundi ya watu wanaodaiwa kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu, waliopanga maandamano kushinikiza kuachiwa kwa viongozi wao.

Kisiwani Zanzibar vurugu kubwa ziliibuka baada ya kusambaa taarifa kuwa Kiongozi wa Kundi la Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed alitekwa nyara juzi saa 3 usiku akiwa kwenye gari lake na dereva wake.

Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa mali kadhaa ikiwamo Maskani Kaka ya Kisonge inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilichomwa moto na waandamanaji.


Waandamanaji hao pia walichoma moto baa za Darajani na Mbawala eneo la Mikunguni na baadhi ya nyumba za kulala wageni, kabla Vikosi vya Kutuliza Ghasia (FFU) na Kikosi cha Zima Moto kudhibiti vurugu hizo kwa mabomu ya kutoa machozi.

Pia magari kadhaa yalichomwa moto na kuharibiwa vibaya yakiwa yameegeshwa katika maeneo mbalimbali, huku mipira na matairi vikichomwa katika barabara kadhaa.

Katika maeneo ya Mjini baadhi ya njia zilifungwa na watu waliokuwa wakitoka kazini walishindwa kwenda nyumbani. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni yale ya Malindi, Darajani hadi Michenzani ambako njia zilifungwa na mabomu yalisikika yakipigwa mfululizo.

Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheik Abdallah Said alisema,
“Taarifa tulizonazo ni kwamba Sheikh Farid ametoweka katika mazingira ya kutatanisha…Alitoka kwake Mbuyuni katika gari yeye na kijana wake wa hapo nyumbani, lakini baadaye kuna gari ikamfuata na kusimama na ndipo alipoingia katika hilo gari jingine na hakuonekana tena. Hatujui ni kina nani waliomchukua na hatujui ilikuwaje akaingia katika hilo gari ...” 

Polisi waliimarisha ulinzi katika baadhi ya maeneo hasa Msikiti wa Mbuyuni ambao uko jirani na makazi ya Sheikh Farid. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema polisi halihusiki na kukamatwa kwa Farid, lakini wao wanaamini kwamba ‘amejipoteza’ mwenyewe na kujificha.

Kamishna Mussa alisema polisi watawasaka wote waliosababisha vurugu hizo, na kwamba hadi sasa hawafahamu chanzo chake bado.

“Tunafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha fujo hizo ingawa mimi sijui habari za kutekwa Farid, sasa tunasema tunachunguza chanzo cha vurugu hizo na tukishapata uthibitisho na waliosababisha tutawafikisha mahakamani kujibu mashtaka,” alisema kamishna huyo.

Ilivyokuwa Zanzibar
Vurugu hizo zilianza katika maeneo mbalimbali muda mfupi baada ya vijana kadhaa kukusanyika katika eneo la Darajani kando ya Soko Kuu majira ya asubuhi, kutokana na kuzagaa kwa taarifa kwamba Sheikh Farid alikuwa haonekani.

Idadi ya vijana hao ilikuwa ikiongezeka kadiri muda ulivyosonga, huku wengi wao wakiwa na silaha za aina mbalimbali zikiwamo magongo na mawe, hali iliyoibua hofu kwa wafanyabiashara wa eneo hilo, hivyo baadhi yao waliamua kufunga maduka.

Maeneo yalioharibiwa ni pamoja na baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zimechomwa moto katika eneo la Amani, huku baadhi ya vijana wakionekana wakikimbia na kreti za pombe.

Katika eneo la Darajani, vijana kadhaa wakishirikiana na Wamachinga, walionekana wakivunja kisha kuingia katika moja ya maghala ya kuhifadhia bia, ambako walipora bidhaa zote zikiwamo kreti kadhaa za bia zilizokuwa zimehifadhiwa humo.

Baadhi ya wenye maduka walifunga na kutoweka, lakini waporaji waliiba baadhi ya bidhaa vikiwamo vyakula, kisha  kutokomea navyo kusikojulikana.

Katika maeneo ya Ng’ambo ambayo ni Amani, Mikunguni, Kwerekwe na Daraja Bovu vijana walioonekana kuwa na hamasa, waliingia kwenye makazi ya watu na kuiba vitu kadhaa, na kila mabomu yalipopigwa walikimbilia vichochoroni na baada ya muda walirejea tena.

Maeneo ya Malindi, Michenzani na  Rahaleo, kulikuwa na vurugu za urushaji mawe na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo hayo.

Matawi ya miti ilikatwa na kuunganishwa na magari mabovu kuwekwa barabarani kisha kuchomwa moto. Hali hiyo ilisabababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya barabara, na katika fujo hizo baadhi ya vijana walikamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed alithibitisha kutokea kwa fujo hizo na kusema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kujua chanzo chake na taarifa kamili zitatolewa baada ya kukamilika uchunguzi huo.

Ponda Dar  
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu walipanga kufanya maandamano hadi Makao Makuu ya Polisi, kupinga kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda aliyekamatwa juzi usiku na kushikiliwa kutwa nzima ya jana katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Ponda alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani jijini Dar es Salaam, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisisitiza kuwa polisi wamechoka kuvumilia harakati zake za kutaka “nchi isitawalike”. 

“Kuanzia leo uvumilivu kwa Jeshi la Polisi dhidi ya watu wasiofuata sheria za nchi umekwisha. Kwa kuwa Ponda ni mtu anayepotosha watu waliopo chini yake wanaotaka kuandamana bila utaratibu wasitulaumu kwa lolote lile litakalotokea,” alisema Kova.

Kova alisema hadi jana Ponda alikuwa bado anahojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba ushahidi ukijitosheleza, atafikishwa mahakamani wakati wowote.

Alisema taasisi anayoingoza Sheikh Ponda haijasajiliwa kwa mujibu wa sheria kufanya shughuli za dini. Hivyo basi shughuli zote zinazoendesha na taasisi hiyo si halali.

"Natoa wito pia kwa wafuasi wa kiongozi huyo, walioshiriki katika vurugu mbalimbali za hivi karibuni, wajisalimishe haraka kwa kuwa sasa tupo katika mchakato wa kuwasaka, kuwakamata na baadaye kuwafikisha mbele ya sheria," alisema.

Tuhuma za Ponda
Kamanda Kova alidai kuwa Sheikh Ponda amekuwa akichochea vurugu na kuwashawishi wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.

“Ponda amekuwa ni mtu ambaye amefanya nchi hii, hasa katika Jiji la Dar es Salaam kukaa katika hali ya wasiwasi. Ijumaa imekuwa siku ya fujo badala ya kuwa siku ya amani,” alisema Kova.

Alisema vurugu hizo zinazoongozwa na Sheikh Ponda zimekuwa zikisababisha baadhi ya watu kushindwa kwenda kazini siku za Ijumaa na hali hiyo haivumiliki tena.

Kamanda Kova alitaja tuhuma nyingine dhidi ya Sheikh Ponda kuwa ni kuongoza kundi la watu kwenda kuvamia kiwanja namba 311/3/4 eneo la Chang’ombe ambacho kinamilikiwa  na kampuni Agritanza.

"Kiwanja alichokwenda kukivamia kilikuwa mali ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) na kiliuzwa kihalali kwa kampuni hiyo," alisena.

Alitaja tuhuma nyingine kuwa ni kufanya maandamano kinyume cha sheria, ikiwamo kuweka kambi Makao Makuu ya Polisi bila kibali cha jeshi hilo wiki kadhaa zilizopita.

Kamanda huyo alisema Ponda anashikiliwa pia kwa kuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola  na Serikali, ikiwa ni pamoja na kushawishi wafuasi wake kumdharau Rais wa nchi.

“Vilevile amekuwa akiendesha maandamano na kukusanyika Kiwanja cha Kidongo Chekundu, huku wakijitapa kuwa wana nguvu zaidi ya Jeshi la Polisi,” alieleza Kova.

Polisi pia wanamtuhumu Ponda kwa kuanzisha vurugu na vitisho dhidi ya Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mufti Shaaban Bin Simba na kutaka kumtoa madarakani kwa nguvu pamoja na kutaka kuvamia ofisi yake.

Alikamatwaje?
Kamanda Kova alisema Ponda alikamatwa na askari waliomuwekea mtego kutokana na yeye kuwa bingwa wa kutoroka kila akifanya matukio.

“Askari waliowekwa maalumu kwa ajili ya kumkamata walifanikiwa kumtia nguvuni saa 4:00 usiku karibu na eneo la maficho yake ambako alipelekwa na pikipiki,” alisema Kova.

“Hivi Ponda ni nani mpaka awe na uwezo wa kumpa Rais aliyechaguliwa na wananchi siku saba kuwaachia watu waliopo mahakamani yeye amechaguliwa na nani kuongoza taasisi aliyonayo na anatoa wapi nguvu za kufanya mambo yote hayo?,” alihoji Kova.

Alisema kulingana na matukio anayoyaongoza Ponda, wananchi wameanza kuona kama anaogopwa na vyombo vya dola, jambo ambalo siyo kweli.

Aliongeza kuwa polisi wana uwezo wa kumdhibiti, isipokuwa walikuwa wanatumia busara tangu alipoanza vurugu na kwa sasa uvumilivu umewashinda, hivyo wataanza kumshughulikia.


Kukamatwa kwa Sheikh Ponda kulizua vurugu jijini Dar es Salaam na kufanya baadhi ya wakazi wake hasa maeneo ya Mnazi Mmoja na Kariakoo, kuingiwa kiwewe baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwasambaratisha watu waliokuwa wanataka kuandamana kwa lengo la kushinikiza kiongozi huyo aachiwe.

Hali hiyo ilisababisha watu kukimbia ovyo katikati ya iji na kuongezeka kwa misongamano ya magari, jambo lililofanya usafiri wa daladala kuwa mgumu kwenda na kutoka katikati ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka yao wakihofia kuporwa mali wakati wa vurugu hizo, baada ya vibaka kujichanganya wakijaribu kufanya uhalifu huo.

Katika eneo la Mnazi Mmoja, polisi walirusha maji ya kuwasha kusambaratisha kundi la watu hao, huku wengine wakiwa wanadhibitiwa walipokuwa wakienda Makao Makuu ya Polisi ili kumtoa kiongozi huyo.

Baadhi ya mashuhuda walisema, mbali na Ponda watu hao walikuwa wanataka kwenda polisi kuwatoa watu waliokuwa wanashikiliwa kituoni hapo kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuharibu makanisa katika Kata ya Mbagala wilayani Temeke.


Imeandikwa na Salma Said, Zanzibar, Zaina Malongo na Festo Polea, Dar.


CHANZO : MWANANCHI

No comments:

Post a Comment