MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), amelazimika kuingilia kati sakata la jengo la Makao Makuu ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kutaka kupigwa mnada kwa amri ya mahakama kutokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani na Kampuni ya Leisure Tours and Holdays Limited.
Kampuni hiyo imeomba mahakama hiyo iamuru jengo hilo liliko Mtaa wa Ohio, Dar es Salam lipigwe mnada ili kufidia deni lake inalodai ATCL, dola 716,259.25 za Marekani (zaidi ya Sh1 bilioni), kwa kulikodishia magari mwaka 2008.
Kutokana na ATCL kushindwa kulipa deni hilo kama walivyokubaliana nje ya mahakama, kampuni hiyo iliwasilisha maombi Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara na mahakama iliamuru kampuni hiyo ifanye uthamini wa jengo hilo na kuwasilisha taarifa hiyo.
Mahakama hiyo ilitarajiwa kutoa amri ya kama jengo hilo lipigwe mnada jana, lakini AG aliwasilisha maombi akitaka naye ajumuishwe kwenye kesi hiyo.
Kwa mujibu wa maombi hayo, AG anadai kuwa ameamua kuingilia kati sakata hilo ili kulinda maslahi ya Serikali, kwa kuwa jengo hilo ni mali yake.
Kutokana na maombi hayo ya AG, mahakama hiyo ililazimika kuahirisha kutoa amri yake, badala yake ilipanga kusikiliza maombi ya AG Machi Mosi.
No comments:
Post a Comment