Madaktari waliponiambia kuwa watoto wangu wameungana nilichanganyikiwa, niliona dunia imenigeuka, sikuwahi kuwaza nitakutana na kitu cha namna hii katika maisha yangu.”
Ni maneno ya binti kutoka kabila la Wandali ambalo asili yake ni Mbeya, Grace Joel (19), ambaye Februari 20 mwaka huu, alijifungua mapacha wa kiume ambao wameungana katika sehemu ya kiunoni.
Mwanadada huyo anasema hakuamini macho yake pale madaktari wa Hospitali ya Uyole iliyopo mkoani humo walipomwambia kuwa watoto wake wameungana na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kwenye Hospitali Kuu ya Mkoa wa Mbeya.
"Wakati wa ujauzito wangu sikuwahi hata siku moja kuhisi kuwa ningeweza kuzaa watoto wakiwa kwenye tatizo hili, sikuwahi kuumwa zaidi ya kuvimba miguu tu na hiyo ni hali ya kawaida kwa mjamzito yeyote." anasema Grace ambaye kwa sasa anahitaji msaada wa hali na mali ili kuokoa maisha ya watoto wake.
Licha ya umri huo mdogo, amejikuta kwenye hali ya mateso na uchungu mwingi baada ya familia yake, hususani mume wake, Erick Mwakyusa kumtelekeza kwa kile alichodai kuwa hana haja na watoto walioungana.
"Nilishangaa, familia yangu kunitelekeza katika hali hii baada ya kugundua watoto wameungana, mume na familia yake alinitamkia wazi kuwa hawana shida na watoto walioungana, alisema hawezi kuwalea kwa kuwa kwao hakuna watoto wenye ulemavu wa aina hiyo,” anasema.
"Siyo siri nilisijikia uchungu, sikuamini kuwa mume wangu angenifanyia hivyo, siyo yeye tu hata familia yao yote sikudhani kama wangenigeuka hivyo, nashukuru kwa upande wa familia ya wazazi wangu walikuwa pamoja nami ingawa ni maskini na hawana uwezo wa kunisaidia.
"Hospitali ya Kyela ndiyo iliyonipeleka ile ya Rufaa Mbeya ambao nao walivyoona hali ya watoto wangu wakanishauri kuja Muhimbili, sikuwa na uwezo wa kufika hapa, lakini nawashukuru madaktari wa Rufaa Mbeya walioniwezesha kufika hapa.
Grace anasema watoto wake hao, Elikana na Eliud aliwazaa wakiwa na uzito kilo tano na nusu na walifika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki mbili tangu kuzaliwa kwao.
Wanatumia njia moja kujisaidia
Dk Zaituni Bokhari, ambaye ni Daktari Bingwa katika Kitengo cha Upasuaji kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, anasema kutokana na namna walivyoungana, wanatumia njia moja kujisaidia.
"Njia ya kukojolea wanatumia moja na pia njia ya haja kubwa wanatumia moja, tutakapowatenganisha kuna utaalam ambao utafanywa ili kila mtu aweze kutumia njia yake mwenyewe bila athari zozote," anasema.
Anaeleza kwamba, iwapo upasuaji huo utafanikiwa watoto hao watakuwa kule India kwa wiki mbili ndipo watarejea nchini na kuendelea na matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa Hospitali ya Muhimbili hadi pale afya zao zitakapoimarika.
Kutokana na hali ya kiuchumi ya mama huyo, Dk. Bokhari amewataka wasamaria wema kujitokeza na kutoa misaada mbalimbali kama ya maziwa, nguo na fedha kwa ajili ya vitu vidogo vidogo ili aweze kuwahudumia vyema watoto wake.
Dk. Bokhari anasema wao waliwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya kutokana na uchovu wa safari kwa basi kutoka Mbeya na walikuwa na maambuzi sehemu mbalimbali.
“Walikuwa ni wachanga kabisa, walikuwa na wiki mbili, walikuwa wamechoka kutokana na mwendo mrefu wa basi kutoka Mbeya, walikuwa na homa kali na matatizo katika njia ya kupumua, tukatibu kwanza matatizo hayo ndiyo vipimo vingine vikaendelea,” anasema.
"Wamefika hapa hawakuwa hata na nguo za kutosha, huyu mama naye alikuja katika hali ya kuchanganyikiwa ukizingatia ukweli kuwa ndugu zake wamemtelekeza, tumefanya kazi kubwa sana ya kumpa ushauri nasaha mpaka akakubalina na hali halisi.
"Kuna wakati alikuwa anasema anataka kuondoka awaache watoto kwetu, hali hiyo ilitokana na kuchanganyikiwa, muda mwingi alikuwa akilia ila kwa sasa namshukuru Mungu yeye na watoto wanaendelea vizuri,” anasema.
Kwa nini wameungana
Dk Bokhari anasema hali ya watoto kuungana siyo ya kurithi kama yalivyo kwa baadhi ya magonjwa.
"Hali hii inaweza kusababishwa na upungufu wa madini,” anaeleza.
Mtaalamu mwingine wa afya ameiambia Mwananchi kuwa, “Mapacha wanaofanana kwa kawaida hutokana na yai lililopandikizwa kujigawa mara mbili, baada ya siku 12 mgawanyiko wa seli (chembe chembe) unakuwa umeanza kujipanga kwa ajili ya kujiachanisha katika uumbwaji wa viungo au ogani mbali mbali za mwili”.
Anasema kuwa, jinsi siku zinavyozidi kusogea mgawanyiko wa mapacha kujiachanisha na kujitegemea ikitokea kabla ya seli kufikia wakati wa kuruhusu jambo hilo, ngozi nyembamba za mapacha hao huendelea kuungana na kushikamana.
“Hata hivyo kwa sayansi ya tiba chanzo kikuu hasa hakijulikani,” anaeleza mtaalam huyo.
Matibabu ni India pekee?
Dk Bokhari anasema kutokana na aina ya upasuaji wa watoto hao, inabidi ufanyike kwenye nchi zenye watalaamu na vifaa vya kisasa kama India au Afrika Kusini.
"Upasuaji huu unatakiwa ufanywe na madaktari zaidi ya saba na kila daktari atakabiliana na kiungo chake, mimi pia ni miongoni mwa madaktari ambao nitashiriki upasuaji wa watoto hawa na inatakiwa umakini wa hali ya juu,” anasema.
Anaeleza kuwa, upasuaji wa aina hiyo unaweza kufanyika kwa saa 24 ama chini ya hapo.
SOURCE: MWANANACHI
No comments:
Post a Comment