.

.

.

.

Wednesday, September 17, 2008

Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuph Makamba akihojiwa na waandishi
.Waziri wa Utawala Bora,Sophia Simba
Waziri adaiwa kumkunja shati mgombea UWT
.Asema amechoka na siasa za chuki na mapambano
.Makamba: Mimi siyajui hayo nipo Lushoto
.Wanaotumia vijisenti wapigwa mkwara mzito
Na Mwandishi Maalum,Dodoma
BAADA ya kutulia kwa vuta ni kuvute katika jumuiya ya vijana, Chama cha Mapinduzi (CCM) sasa kimeingia kwenye msukosuko mwingine wa mchakato wa kupata wagombea uongozi wa Jumuiya ya Wanawake (UWT).
UV-CCM ilikitikisa chama hicho baada ya baraza lake kuu kumvua uanachama mwanasiasa chipukizi, Nape Nnauye na kufanya kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kusubiriwa kwa hamu na kundi linalomuunga mkono, kabla ya Rais Jakaya Kikwete kukinusuru chama kwa kumpa mtoto huyo wa mwanasiasa wa zamani, Moses Nnauye, haki yake ya kutumia chama kupinga maamuzi ambayo anayaona hayamridhishi.
Huku wanachama wakianza kulipa kisogo sakata hilo, hali inaonekana bado tata baada ya vigogo wa UWT kukaribia kukunjana, baadhi wakifanya kampeni kwa kuitana malaya, huku makundi yakianza kujionyesha.
Mjini Dodoma, mpasuko umeanza kujionyesha mapema miongoni mwa wanawake katika kikao cha baraza kuu la umoja huo. Hata kabla mkutano haujaanza jana, kundi la wenyeviti wa umoja wa wanawake wa mikoa lilikutana kwa dharura katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuweka mkakati wa pamoja ili kumuunga mkono mwenzao.
Kundi hilo, lilikutana kwa muda mfupi na kuonekana wakiweka mikakati ambayo inaonekana ni ya kumuunga mkono mmoja wa wagombea wanaodaiwa kupambana wakati wa kikao cha Kamati ya Siasa ya mkoa wa Dar es salaam.
Huku hali ikionekana kuanza kuchafuka zaidi, mwenyekiti anayemaliza muda wake, Anna Abdallah alilazimika kutoa karipio dhidi ya vitendo vinavyoonekana kuelekea kukichafua chama.
Mwenyekiti huyo aliwapiga madongo wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya umoja wao, kukemea kitendo cha kuitana malaya, kwa kile alichodai kuwa miongoni mwa wanawake waliokuwemo ndani ya ukumbi huo hakuna asiyejua kuwa uzazi unatokana na tendo la kujamiiana, hivyo hakuna sababu ya kukashifiana
“Hatujapitisha majina ya wagombea na mtu anayepigia watu simu na kudai kuwa wasipomchagua mtu wao kuwa watamkoma, anashangaza. Kwa hakika wanaotakiwa kukukoma ni mumeo na wanao,” alisema waziri huyo wa zamani wa afya.
Kutokana na hali hiyo, Abdallah alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa wanawake kukomesha tabia hizo mbaya za kutafuta uongozi kwa njia za kujengeana chuki, huku akikazia kuwa mtu yeyote anayegombea uongozi na kushinda kwa sifa yake ni kiongozi bora kuliko ikilinganishwa na kiongozi anayeshinda kwa fedha ni mamluki ambaye hataisaidia UWT.
Pia Mwenyekiti huyo alisema kuwa ni muhimu kwa wanachama wa UWT kuhakikisha wanaheshimiana wote na waache kupakana matope, kwani kufanya hivyo hakuna faida yoyote kwa UWT na wanachama wake.
Abdallah alisema kuwa wakati huu anapoelekea kulitua zigo la uongozi huo, huku mchakato wa uchaguzi ukiwa umeanza, ni muhimu sana kuipatia UWT viongozi mahiri na bora, na kwamba katika hali hiyo ni bora wanachama waachiwe kumchagua mtu wanayempenda na pia iwe kwa utashi.
Mwanasiasa huyo mkongwe pia alikemea rushwa akisema: “Nasikia kuna vijisenti vinatembea, rushwa jamani iacheni, vinginevyo mtaingiza watu kwa maslahi yao. Wengine wanadhani rushwa itawasaidia kupita, katu haitasaidia.”
Mapema wiki hii iliripotiwa kutokea mtafaruku mkubwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa cha UWT mkoani Dar es salaam wakati mwenyekiti jumuiya hiyo mkoani Dar es salaam, Janeth Kahama alipopambana na Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba kwenye kikao hicho kwa tuhuma za kuchafuana.
Wakati tayari Kahama amenukuliwa na vyombo vya habari akisema amemshtaki Simba, kwa Rais Jakaya Kikwete, kutokana na mtafaruku huo, waziri huyo mwenyewe naye ameunguruma akisema hoja ya msingi imepotoshwa.
Simba alisema mchakato huo wa kupata wagombea umetawaliwa na chuki na rushwa na kusisitiza kwamba, yeye kama mwanasiasa makini asingependa siasa za malumbano.
"Nimechoka hizi siasa za chuki na mapambano yasiyo na msingi hazina mana... nimechoka. Mimi ni mwanasiasa makini, kwanini nilumbane na kupambana katika siasa zisizo na msingi" alihoji Simba.
Simba alifafanua kuwa siku ya mkutano alijaribu kuwasilisha malalamiko yake ya msingi ambayo ni kuonya kuhusu rushwa ya wazi ambayo inafanyika katika mchakato huo, hata hivyo, hilo likageuzwa na kuelezwa yeye kutaka kufanya vurugu.
Alipoulizwa ilikuwaje waziri anayehusika na utawala bora kutaka kuvutana mashati na mwenzake tena mbele ya kadamnasi, alijibu: "Huo ni uongo, mimi nilipeleka malalamiko yangu katika kikao mahususi cha Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa, hiyo haikuwa kadamnasi.
"Kile kilikuwa ni kikao na nililalamika rushwa ya wazi anayofanya mmoja wa wenzangu, lakini hilo halisemwi."
Kauli hizo za waziri Simba na za Kahama, ambazo tayari amezitoa baada ya kuulizwa kuhusu sakata hilo, zinaonyesha CCM iko katika wakati mwingine mgumu kuweza kupata suluhu ya hali ya mambo ndani ya jumuiya hiyo.
Katika sakata la UV-CCM, Nape aliingia kwenye kampeni za uenyekiti kwa kishindo alipotuhumu vigogo wa chama kuhusika katika kuisaini mkataba ambao hauna maslahi kwa UV-CCM katika uwekezaji wa jengo la makao makuu.
Mwenyekiti wa UV-CCM, Emmanuel Nchimbi, katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa walijikuta katikati ya tuhuma hizo na busara za Rais Kikwete ndio zilituliza pande zote.
Naye Makamba, ameonya kwamba chama kupitia Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) havitakubali kuona taratibu zikikiukwa.
Akizungumzia zaidi mchakato huo, Makamba alisema katika mkutano wa NEC uliofanyika wiki iliyopita mkoani Dodoma, walipokea taarifa mbalimbali za mchakato wa uchaguzi wa jumuiya zote, ambazo zilionyesha unakwenda vizuri.
Hata hivyo, Makamba alifafanua, katika taarifa hizo NEC ilionya kwamba mgombea yeyote ambaye atatumia ushawishi kwa kuhonga wagombea au kukiuka taratibu kwa namna yoyote, hata kama atashinda, jina lake litakatwa ndani ya jumuiya na huo ndiyo msimamo wa chama.
Alipoulizwa anachukuliaje kitendo cha Waziri Simba na Kahama kupambana, alijibu: "Mimi sikuwepo, mana tangu juzi niko huku Lushoto, hilo sijalifahamu."
Ukiacha Simba na Kahama, mwingine anayewania kuchaguliwa UWT ni Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto Magareth Sitta.
Awali Mwenyekiti huyo amewatangaza wajumbe wa baraza kuu la UWT waliochaguliwa na wajumbe wenzao wa NEC kutoka miongoni mwa wajumbe 58 wa halmashauri kuu wanawake.
Aliwataja wajumbe hao kuwa ni pamoja na katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Maudline Cyrus Castico, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Utawala bora, Sophia Simba, naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii, Dk Aisha Kigoda, mbunge wa viti maalum na mjumbe mwingine ni Subira Mzabe.

No comments:

Post a Comment