.

.

.

.

Friday, October 31, 2008

EPA IMEKUWA HAIEPEKI


Ukisikia namna ile mijamaa iliyojichotea mabilioni ya pesa kutoka Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje, EPA ilivyohaha jana kurejesha pesa hizo kabla ya kipenga kupulizwa leo, walahi utadhani ni simulizi za kubuni za elfu lela ulela! Ilikuwa patashika nguo kuchanika kwenye mabenki. Kwa mahesabu ya haraka haraka, inadaiwa kwa jana tu, shilingi 17,000,000 zililerejeshwa. Habari za kuaminika zinadai kuwa, mapesa hayo yalibwagwa benki jana alasiri na kutokana wingi wake, makarani wakayahesabu hadi usiku wa manane. Kwa mujibu wa taarifa toka kwenye tawi la benki moja maarufu Jijini (jina linalihifadhiwa), mapesa hayo yaliyokuwa kwenye maboksi ya mbao, mengi yakiwa ya noti za alfu kumi-kumi na alfu tano. ``Haikuwa kazi rahisi. Noti zenyewe zilikuwa ni nyingi mno na zilifikishwa katika muda ambao tayari wengine walishachoshwa na shughuli za mchana... wakajikuta wakikesha kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo ambalo lilianza muda mbaya wakati benki zinakaribia kufungwa,`` kikadai chanzo chetu. Imedaiwa kuwa mmoja wa wahusika hao alirejesha kiasi cha shilingi bilioni 12 taslimu na mwingine akarejesha bilioni tano. Watu hao ni miongoni mwa waliokuwa wakitajwa tajwa kujichotea mapesa hayo. Imedaiwa kuwa pesa hizo zilifikishwa katika tawi la benki hiyo zikiwa katika magari mawili ambayo yalifika kwa nyakati tofauti na kupakua maboksi yaliyosheheni minoti hiyo. Urejeshwaji huo wa staili ya aina yake, ulifanyika zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kufika tarehe ya mwisho aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete kwa waliochota pesa hizo kuwa wamezirejesha.

No comments:

Post a Comment